Home Makala BAADA YA KUTAKATA KWENYE LIGI YA MOROCCO…MSUVA HUYOOO ULAYA…AITAJA LA LIGA YA...

BAADA YA KUTAKATA KWENYE LIGI YA MOROCCO…MSUVA HUYOOO ULAYA…AITAJA LA LIGA YA HISPANIA…

 


ZIPO ligi nyingi na kubwa barani Ulaya lakini fikra na mawazo ya Mtanzania, Simon Msuva ambaye anakipiga huko Morocco kwenye klabu ya Wydad Casablanca ni kucheza Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

Kwanini La Liga? Msuva ambaye siku chache zilizopita alikuwa nchini kwa mapumziko, alisema ni kutokana na soka la Hispania kuendana na Morocco.

“Niliwahi kwenda Hispania nikiwa na Difaa wakati huo nikiwa mchezaji mgeni huku Morocco, ilikuwa ni ziara ya kujiandaa na msimu uliokuwa ukifuata wa Ligi, tumepakana nao ndio maana ilikuwa rahisi kwetu kwenda huko, tulipata michezo kadhaa ya kirafiki na hapo ndio niliamini kuwa wanaendana,”

“Hata kama utoafuti upo basi ni mdogo sana, nilifurahia sana ziara ile na niliingia na shauku sana ya kutamani kupata nafasi ya kucheza soka Hispania kwa sababu ni taifa zuri na shindani kati ya zile ligi kubwa zaidi Ulaya,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.

Msuva aliongeza kwa kusema kuwa na ndoto ya kucheza Hispania haina maana kuwa ikitokea nafasi ya kucheza Ujerumani, Ureno, Ufaransa au England anaweza kukataa.

“Mimi ni sawa na mkulima, si sawa kabisa kuchagua jembe, Ligi ya Morocco imenifanya kupiga hatua nyingine, najiona kuwa mpya kila siku hivyo naamini popote ambako naweza kupata nafasi siwezi kusita kuchangamkia, kwa sasa nguvu zangu nimezielekeza kufanya vizuri nikiwa na Wydad.”

Huu ni msimu wa tano kwa Msuva kucheza Ligi Kuu Morocco ambayo ni maarufu kama Batola Pro, misimu mitatu alikuwa na Difaa El Jadida na kutupia mabao 29 kwenye michezo 49, ndani ya msimu wake wa kwanza hakuonyesha kuwa ni mgeni kwenye ligi hiyo kwani alitupia mabao 11.

Msuva ametupia mabao 48 na kutoa asisti 17 kwenye mashindano yote ndani ya misimu yake mitano ya kucheza soka la kulipwa nchini humo, nyota huyo wa Kitanzania ni kati ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi hiyo wenye wastani mzuri wa kupachika mabao.

SOMA NA HII  KWA KAULI HII YA AJABU YA MWAKALEBELA KUHUSU CAF...INADHIHIRA MAWAZO NA MITAZAMO YA YANGA KWA UJUMLA...