Rasmi, Klabu ya Simba hivi karibuni itamtangaza Masau Bwire kuwa Afisa Habari wake akichukua nafasi ya Ezekiel Kamwaga ambaye mkataba wake umeisha na sasa yupo London Uingereza kwa masomo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya timu hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, zinasema kuwa ndani ya siku kadhaa nyuma Masau Bwire amekuwa na vikao vingi vya kujadili makubaliono ya kazi na waajiri wake wapya.
Masau Bwire ambaye anasifika kwa tambo na maneno ya ‘shombo’ pindi waliokuwa na waajiri wake wa awali Ruvu Shooting walipokuwa wakicheza na timu pinzani, inadaiwa amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuhudumu kwenye Klabu ya Simba kwa nafasi ya Afisa Habari.
Chanzo cha habari hii pia kimeihakikishia Soka la Bongo kuwa Masau anaweza kutangazwa aidha kabla ya mechi dhidi ya Yanga au baada ya mechi, huku suala zima la kusaini mkataba likiwa limeshamalizika.
Hata hivyo, katika mtandao wake wa kijamii, Masau Bwire hivi karibuni ameweka picha akionekana akiwa ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez huku kukiwa na karatasi ambayo inasemekeana ni sehemu ya Mkataba wake wa kazi.
Kwa miezi ya hizi karibuni pia Masau Bwire pamoja na kuwa alikuwa msemaji wa Ruvu Shooting, lakini alikuwa akitumia ukurasa wake wa Instagram kuipamba Simba na kuhamasisha mashabiki wa timu hiyo yenye mafaniko ya uwanjani kwa sasa kwenye Soka la Tanzania.
Kuajiriwa kwa Masau Bwire kwenye timu ya Simba kunatazamiwa kuongeza hamasa na kurudisha zile ‘hamsha hamsha’ ambazo zilikuwa zikifanywa na aliyewahi kuwa kwenye nafasi hiyo kabla ya kuhamia yanga Haji Manara.
Masau Mwire anaingia Simba huku jukumu lake la kwanza likiwa ni kuhakikisha anarudisha hamasa kwa mashabiki wa timu hiyo na kuondoa unyonge wa kutambiwa na Haji Manara ambaye toka ahamie Yanga amegeuka kuwa ‘ndimu’ kwenye kila jambo la Simba.
Itakumbukwa kuwa Masau Bwire pia ni mwalimu wa shule ya msingi ya Serikali mkoani Pwani kazi ambayo amekuwa akiifanya hata alipokuwa msemaji wa Ruvu Shooting, hivyo kuajiriwa kwake Simba pengine kunaweza kukamfanya akaiacha kazi hiyo, au akaifanya kwa makubaliano maalumu na waajiri wake wapya.