Home news PAMOJA NA MAFANIKO YOOTE WALIYONAYO…HIVI NDIVYO YANGA INAVYOZIDI KUIKIMBIZA SIMBA…

PAMOJA NA MAFANIKO YOOTE WALIYONAYO…HIVI NDIVYO YANGA INAVYOZIDI KUIKIMBIZA SIMBA…


SIMBA na Yanga zinachuana katika msimamo wa Ligi Kuu Bara iliyoingia raundi ya 10, kila mmoja ikiupigia hesabu ubingwa wa msimu, lakini vijana wa Jangwani wakionekana kuwazidi ujanja watani wao mpaka sasa, licha ya tambo zilizozagaa mtaani.

Achana na Yanga kuwa ndio vinara wa kubeba mataji mengi ya ligi, ikifanya hivyo mara 27 dhidi ya 22 ya Simba, lakini unaambiwa vijana hao wa Jangwani wameiacha mbali kwa sasa katika rekodi za kucheza mfululizo bila kupoteza mchezo kwenye ligi hiyo.

Gazeti la Mwanaspoti limeipekenyua ligi ya msimu huu na ile iliyopita na kubaini kwamba Yanga imefikisha jumla ya mechi 16 bila kupoteza mchezo hadi sasa wakati watani wao wana mechi 12 tu.

Kama hujui ni kwamba mara ya mwisho kwa Yanga kufungwa kwenye ligi ilikuwa April 25 mwaka huu walipotunguliwa bao 1-0 na Azam katika mechi tamu ya msimu uliopita iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa bao lililofungwa na Prince Dube.

Baada ya mechi hiyo, Yanga ilikuwa ikipata matokeo ya kushinda na sare tu, ikicheza mechi saba za msimu uliopita bila kufungwa na kuziongea tisa ilizocheza msimu huu ikikaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 23 na mabao 14 ya kufungwa na kuruhusu matatu nyavuni mwao.

SIKU 243

Kimahesabu inaonyesha kuwa Yanga imekaa siku 243 bila kuonja machungu ya kupoteza tangu pale Prince Dube alipomtungua kipa, Faruk Shikhalo katika dakika ya 86 ya mchezo wao wa marudiano ya msimu uliopita.

Kifupi unaweza kusema, Azam ndio timu ya mwisho kuitungua Yanga katika Ligi Kuu Bara, licha ya mabingwa hao wa zamani walimaliza kwenye nafasi ya pili ikikusanya pointi 74 katika wemchi zao 34, ikishinda 21 na sare 11, huku ikipoteza mechi mbili tu. Ukiachana na hilo, katika mechi za msimu huu, Yanga imecheza mechi tisa, ikishinda saba na kupata sare mbili zilizoifanya ivune alama 23 na mabao 14.

SIMBA SASA

Kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi, Simba tangu ilipotunguliwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya Kariakoo Derby iliyopigwa Julai 3, timu ikiwa chini ya Didier Gomes, haijapoteza tena katika ligi na kukamilisha idadi ya mechi 12, zikiwamo nne za msimu uliopita na nane za msimu huu.

SOMA NA HII  KOCHA MPYA YANGA AANZA VURUGU HUKOO...APIGA STOP WACHEZAJI WAZEEE...MASTAA TUMBO JOTO..

Hesabu zinaonyesha Simba imetumia siku 175 bila kufungwa kabla ya juzi kushuka uwanjani kuvaana na KMC katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora.

Pamoja na maumivu hayo, bado Simba ilinyakua ubingwa wa msimu uliopita kwa kukusanya pointi pointi 84, katika mechi 34, ikishinda 26, sare tano na kupoteza mitano, huku ikifunga mabao 78 na wenyewe kuruhusu 14.

Wakati Simba na Yanga zikiwa zinatamba na rekodi hizo, ikumbukwe Azam ndio klabu inayoshikilia rekodi ya kucheza mechi kwa muda mrefu bila kupoteza ikifanya hivyo kati ya mwaka 2012-2014 ikishuka uwanjani mara 38.

Msimu wa 2012-2013 Azam ilipasuliwa na Yanga katika mechi iliyopigwa Februari 23, 2013 na kucheza mechi nane za mwisho za msimu huo bila kupoteza, kisha ikacheza mechi 26 za msimu wa 2013-2014 waliobeba ubingwa kisha kuongeza mechi nne za msimu wa 2014-2015 kabla ya JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania) kuwatibuliwa kwa kuwafunga bao 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani, mechi iliyopigwa Oktoba 25, 2014.

Msimu uliopita Yanga ilijaribu kuifukuzia rekodi hiyo kwa kuchez mechi 32 bila kupoteza akiunganisha mechi 11 za msimu wa 2019-2020 na 21 za 2020-2021 kabla ya Coastal Union kuwatibuliwa Mkwakwani, jijini Tanga.