Home BIashara United KISA MBADALA WA DIARRA…YANGA WAPIGWA BAO LA JIONI…WABAKI ‘KUKODOA MACHO’..

KISA MBADALA WA DIARRA…YANGA WAPIGWA BAO LA JIONI…WABAKI ‘KUKODOA MACHO’..

 


MABOSI wa Yanga walikuwa ameanza kupumua baada ya dili lao la kumnyakua kipa chipukizi mwenye kipaji kikubwa, Abdultwalib Mshery kutoka Mtibwa Sugar, likionekana kutiki, lakini ghafla mambo yamegeukia kutokana na vigogo wa Manungu kuchomoa kumuachia kipa huyo.

Yanga ilikuwa ikiamini Mshery ndiye kipa sahihi wa kuibeba timu yao wakati kipa namba moja, Diarra Djigui atakapoenda na timu yake ya taifa ya Mali kwenye Fainali za Afrika (Afcon) yanayoanza mwezi ujao na ilikuwa imefikia hatua nzuri kwenye dili hilo kabla ya kutibuka dakika za mwisho.

Kabla ya kumfuata Mshery kupitia wakala wake na mchezaji huyo kukaririwa kama mabosi wake watamruhusu yeye anaweza kucheza kokote, ingawa hakutaka kuzungumzia dili hilo kwa vile bado ana mkataba mrefu na timu hiyo ya Manungu, Yanga ilikuwa ikiwapigia hesabu makipa wa Ruvui Shooting, Mohammed Makaka na yule wa Mbeya City, Haruna Mandanda.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga na Mtibwa zinasema dili la Mshery limekufa na kwamba hawezi kutua Jangwani, licha ya awali Yanga kupewa sharti ya kuuvunja mkataba wake Manungu kwa kulipa Sh 20 Milioni kabla ya kukubaliana kimasilahi na kipa huyo kijana.

Yanga ilishamuandalia Mshery mkataba wa miaka miwili wenye donge nono, lakini kauli ya mmoja wa vigogo wa Mtibwa kwa kuiambia Yanga ‘Mshery hauzwi’ imewanyong’onyesha.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alipendekeza usajili wa Mshery kutokana na kuvutiwa na kiwango chake na aliwapa jina hilo mabosi wake.

Inafahamika kuwa baada ya kupewa jina hilo, mabosi wa Yanga wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Injinia Hersi Said ilianza mazungumzo na Mshery aliyekubaliana naye kusaini, lakini ikabaki kwa Yanga na Manungu kumalizana mezani ili apate baraka zote.

Yanga ikapeleka ofa yao kwa Mtibwa, nao waliitana fasta na kuonekana kama wanaikubali kabla ya kigogo wa juu kuzuia dili hilo kwa sababu ya hali mbaya iliyonayo timu hiyo katika ligi.

Moja ya viongozi wa juu kabisa wa Mtibwa ambaye hakutaka kutajwa jina lake liandikwe alisema kuwa, ishu kwao sio pesa, lakini hawawezi kumuachia Mshery kwa hali ya timu yao.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA PETER BANDA KUTIMKIA SAUDI ARABIA...UONGOZI SIMBA WATOA NENO..BARUA YAPOKELEWA...

“Hatumuachii Mshery kutokana na hali ya timu ilivyo, ndiye kipa wetu tegemeo na ukiangalia kwa sasa tupo kwenye nafasi ngumu kwenye ligi hivyo hatumuuzi,” alisema kigogo huyo na kuongeza;

“Ofa yake ilikuwa ni kubwa na ingeongezeka maradufu kama tungemuuza, lakini kwa vile tunamhitaji sana kikosini basi haendi kokote,” alisema.

Mshery alisaini mkataba mpya mwanzoni mwa msimu huu, lakini angeweza kutoka kama mkataba wake ungevunjwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mtibwa, Jamal Bayser alisema Mshery bado ana mkataba na ataendelea kuwepo kikosini, licha ya Yanga kuvutiwa naye.

“Mashabiki wa Mtibwa wanapaswa kuwa watulivu, Mshery ni kijana wetu, ataendelea kuwepo kikosini, hatuna mapango wa kuachana naye kwa sasa,” alisema Bayser, huku Mshery akisema yeye ni mchezaji wa Mtibwa kwani ana mkataba, hivyo anawasikiliza viongozi.

“Sina cha kufanya zaidi ya kuwasikiliza viongozi wangu wameamua nini, maana bado nina mkataba na Mtibwa, hivyo nitafuata kile watakachoamua wao,” alisema Mshery.

YAGEUKIA KIPA WA NJE

Fasta baada ya kugundua ni ngumu kumnasa Mshery, huku wakiwa hawana uhakika na uwezo wa makipa waliowataka mwanzoni yaani Makaka na Mandanda, mabosi wa Yanga wameamua kugeukia nje ya nchi kuleta kipa la maana.

Taarifa za ndani ya Yanga zinadai huenda mabosi wakaamua kutafuta kipa mkali wa kigeni ambaye watampa mkataba wa miezi sita ili kuwa mbadala wa Diarra, huku ikiendelea kuisikilizia Mtibwa kwa Mshery.