Home Makala REKODI ZINAMTESA SALUM KIMENYA WA TANZANIA PRISONS

REKODI ZINAMTESA SALUM KIMENYA WA TANZANIA PRISONS


KUWEKA rekodi ni jambo la kwanza na kuikifikia rekodi ni jambo lingine pia katika ulimwengu wa soka.


Salum Kimenya, nyota wa Tanzania Prisons kwa sasa amebakiza dk 180 ambazo ni mechi mbili kuweza kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita ya kufunga mabao 7 na pasi 7 za mabao.


Huenda inaweza ikawa ngumu kwake kwa kuwa mpaka wakati huu amefunga bao moja pekee na ana pasi tano za mabao.


Machi 10,2021, alipachika bao lake la kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara ilikuwa Uwanja wa Mkapa kwa pigo huru lililomshinda mlinda mlango namba moja wa Simba, Aishi Manula.


Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa baada ya dk 90, ubao ulisoma Simba 1-1 Prisons na kuwafanya wagawane pointi mojamoja na kuwafanya Prisons wasepe na pointi nne mbele ya Simba kati ya sita.


Katika mchezo wa kwanza walisepa na pointi tatu mazima ilikuwa Uwanja wa Nelson Mandela baada ya ushindi wa bao 1-0 ilikuwa ni zama za Sven Vandenbroeck Oktoba 22,2020.


Baada ya mchezo huo Kimenya alikutana na rugu kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kufungiwa mechi tatu kwa kile kilichoelezwa kuwa alimchezea mchezo usio wa kiungwana kiungo wa Simba, Bernard Morrison.


Msimu huu Prisons ikiwa imecheza jumla ya mechi 32 alianza kikosi cha kwanza kwenye mechi 23 ambazo ni sawa na dk 2,070. Ikiwa imebakiza mechi mbili kukamilisha mzunguko wa pili bado haoni kama anaweza kuvunja rekodi yake aliyoweka msimu wa 2019/20 ya kufunga mabao 7 na pasi 7 za mabao.

 Ikumbukwe kwamba msimu wa 2018/19 aliweza kuwa bora kwenye kutengeneza nafasi za mwisho na alikamilisha akiwa na pasi 7.


Huyu hapa Kimenya anafunguka kuhusu msimu wa 2021/22 namba ulivyokuwa kwake na hesabu:-


“Kweli kwangu mimi ninaweza kusema kwamba msimu huu umekuwa ni mgumu tofauti na msimu uliopita ambapo niliweza kufanya vizuri kiasi. Pasi 7 na mabao 7 haikuwa haba ila msimu huu mambo bado.


“Nimefunga bao moja pekee ilikuwa mbele ya Simba na pasi za mabao nimetoa tano, bado sijafikia rekodi yangu ya msimu uliopita.

SOMA NA HII  ALICHOKISEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU NANI BORA KATI YA AISHI MANULA NA DJIGUI DIARRA....


Kipi kilichofanya yote yakatokea?


“Ninaweza kusema kwamba ni matokeo ambayo yanatokea uwanjani kwani wakati mwingine nahitaji kufanya vizuri ila haiwi hivyo kikubwa ninashukuru.


“Pia msimu nilianza nikisumbuliwa na majeraha ambapo nilikuwa ninatibu nyama za paja hivyo kuna wakati nakuwa kwenye kasi halafu siendelei pale nilipoishia kwa kuwa ninakuwa nje ya uwanja.


“Kuna wakati pia nilifungiwa mechi tatu nisicheze hapo kuna mechi nyingine pia nilikosa.


Mechi zipi ambazo unazikumbuka kwa msimu huu?


“Zile ambazo zilitukutanisha dhidi ya Simba na Yanga. Hizi ni mechi kubwa na zinahitaji ushindani mkubwa ukizingatia kwamba wao wana uzoefu pamoja na uwezo hivyo kushinda mbele yao inahitaji maandalizi mazuri na akili katika kupambana nao.


Je kucheza na timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja ipoje?


“Hakuna ugumu ila kunakuwa na presha kubwa kwa timu zote, hasa pale ambapo unahitaji kufanya vizuri na unakutana na timu ambayo nayo inahitaji matokeo hapo ni lazima mpambane kusaka matokeo.


Tofauti ya msimu huu na uliopita je?


“Msimu huu umekuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa ukiondoa Mwadui FC ambayo imeshuka bado timu tatu haijulikani ni zipi mpaka ligi itakapokwisha hivyo mambo ni magumu na ushindani ni mkubwa.


Je mmeweza kufikia malengo?


“Hapana hapa tulipo tupo nje ya malengo kwa kuwa tulikuwa tunahitaji kuwa sehemu nzuri zaidi ya hapa ambapo tupo kwa sasa,” anamaliza Kimenya.