Home news KUELEKEA KARIAKOO DABI…VIKOSI VYA TIMU ZOTE HIVI HAPA…MORRISON KAMA KAWA KULIANZISHA…

KUELEKEA KARIAKOO DABI…VIKOSI VYA TIMU ZOTE HIVI HAPA…MORRISON KAMA KAWA KULIANZISHA…


UBISHI uko hapa! Nani aanze. Mashabiki vijiweni wamechanganyikiwa na makocha nao mazoezini wanakuna vichwa. Mchuano ni mkali kila mmoja anataka namba Kwa Mkapa leo jioni.

Achana na Aishi. Ukiwaangalia Pascal Wawa na Joash Onyango kwenye mazoezi ya Pablo Franco wanavyoupiga mwingi utadhani wamesajiliwa jana wanatafuta namba. 

Lakini kuna fundi mmoja Henock Inonga huyo ndiye usiseme. Katika mazoezi ya wiki amekuwa kwenye kiwango cha juu kama kina Jonas Mkude, Meddie Kagere, Morrison ambao wana mzuka mkubwa wa kuituliza Yanga kesho.

Kigamboni kwa Yanga, huyo Mayele, Fei Toto, Mukoko, Saido, Bangala na Aucho wanakiwasha kwelikweli. Kocha Nabi Mohammed hajui nani aanze nani aende jukwaani. Mtihani mzito wa dabi ya kesho ambayo wachambuzi wengi wamesisitiza hakuna sare wala suluhu.

Gazeti la Mwanaspoti kwa nyakati tofauti limetembelea kambi za timu zote na kubaini ushindani ni mkubwa. Watu hawapati usingizi. Kwa mujibu wa mazoezi mpaka jana jioni kesho wanaweza kuanza hivi;

Simba huenda wakaanza na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Henock Inonga, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Sadio Kanoute, Meddie Kagere, Rally Bwalya na Bernard Morrison.

Benchi pale watakuwepo, Benno Kakolanya, Israel Mwenda, Gadiel Michael, Joash Onyango, John Bocco, Kibu Denis, Erasto Nyoni, Dancun Nyoni na Peter Banda.

Huko Yanga; Piga ua Djigui Diarra anaaanza. Djuma Shabani, Kibwana Shomary, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto wanasimama pale nyuma. Yannick Bangala, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Feisal Salum na Said Ntibazonkiza/Farid Mussa.

Benchi atakaa; Erick Johora, David Bryson, Mukoko Tonombe, Yusuph Athumani, Deus Kaseke, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Yassin Mustapha.

Kiufundi Yanga hawatakuwa na mabadiliko katika eneo la ulinzi ubora alionyesha Diarra kwenye kuokoa mashambulizi na michomo ya wazi pengine ndio maana kikosi hicho kimeruhusu mabao mawili mpaka sasa. Benchi la ufundi linaiamini safu hiyo ya ulinzi pengine kuliko mastraika. Kocha Msaidizi wa Yanga; Cedrick Kaze alisema; “Mwamnyeto, Job ndiyo wachezaji muhimu wanaoona uwanja mzima.”

Diarra amehusika katika bao moja kwenye ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Simba baada kupiga pasi iliyokwenda kwa Farid ambaye alipiga pasi ya mwisho kwa Fiston Mayele aliyepeka kilio Msimbazi.

SOMA NA HII  SKUDU AWAPA NENO HILI WANANCHI KUELEKEA MECHI YA SIMBA vs YANGA

Safu ya ushambuliaji ya Simba yenye Kagere, Morrison, Rally Bwalya na Hassan Dilunga nayo ni moto. Imefunga mabao nane katika ligi huku Kagere ndio akionekana kuwa hatari zaidi kwani amefunga nusu yake huku Bwalya, Dilunga na Kibu kila mmoja akifunga bao moja.

Historia inaonyesha Kagere misimu minne aliyokuwa nchini ameifunga Yanga mara mbili kwenye ligi.

VIUNGO

Yanga wana Khalid Aucho, Yanick Bangala na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anafunga na kutoa pasi za mwisho.

Feisal ameifungia Yanga mabao matatu na kutoa pasi za mwisho mbili huku nyuma yake kuna Bangala na Aucho ambao kazi yao ni kuhakikisha wanakaba mpaka kivuli na eneo hili ndio liliwamaliza Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii.

Katika eneo la kiungo Simba kuna wakati walikuwa wanaanza na Taddeo Lwanga ambaye kwa sasa ni majeruhi, Sadio Kanoute na Rally Bwalya, wakati mwingine huwatumia Dilunga, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu na Mzamiru Yassin.

Ukweli usiopingika viungo wa Simba watakaoanza katika mechi hii wanatakiwa kuwa bora kwenye kukaba na kuficha ubora ule utatu wa Aucho, Bangala na Fei Toto.

Viungo wa Simba mbali ya mabadiliko katika nyakati tofauti nao si wa kuwabeza kwani kuna ambao wanafanya vizuri kupiga pasi za mwisho na kufunga kama ilivyokuwa kwa Dilunga na Bwalya.

Yanga huenda wakawa wanatembea kifua mbele dhidi ya safu yao ya ushambuliaji kwani mbali ya ubora wa Fei Toto, Jesus Moloko na wengineo kuna balaa linaitwa Mayele.

Mayele amekuwa na mwanzo mzuri katika kikosi cha Yanga msimu wake wa kwanza alifunga bao kwenye mechi ya kimashindano dhidi ya Simba ambalo liliipa timu yake ubingwa wa kwanza msimu huu.

Kwa upande wa Simba, Morrison, baada ya kuwabwaga Yanga kule CAS, sasa anatarajiwa kuwavuruga na kumlaza na viatu Djuma Shabani kule kwenye beki ya kulia ya Wanajangwani.

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema Yanga imesajili wachezaji wengi wazoefu ambao wanaukomavu wa kucheza mechi kubwa za namna hii.