Home Makala PAMOJA NA KUANZA KUTAKATA MECHI ZA HIVI KARIBUNI..HAYA HAPA MAMBO 5 YA...

PAMOJA NA KUANZA KUTAKATA MECHI ZA HIVI KARIBUNI..HAYA HAPA MAMBO 5 YA MORRISON USIYOYAJUA..


JINA la winga wa Simba, Benard Morrison, limekuwa kubwa mbele ya wadau wa soka tangu atue Tanzania mwaka 2020 akiichezea Yanga miezi sita, kisha kuhamia Simba kuanzia msimu wa 2020/21.

Ndani ya miezi sita aliyokuwa anaitumikia Yanga iliyomtoa Sauzi akiwa mchezaji huru, umaarufu wake ulitokana na namna alivyofanya kazi ya soka kuwa rahisi hadi alikuwa anapanda juu ya mpira, jambo ambalo lilikuwa linawapa raha Wanajangwani.

Aliimbwa nyimbo tamu na mashabiki wa Yanga, mfano mfuasi kindakindaki wa timu hiyo, Frank Yanga alifikia hatua ya kuandika jina la staa huyo kwenye gari lake, kabla kibao cha kumnanga hakijageuka.

Wakati huo Morrison alikuwa mchungu kwa Simba, alivyowafunga bao 1-0 (2019/20) mechi ya mzunguko wa pili, ambapo mashabiki walikuwa wakimnanga huku wakibeza uwezo wake.

Upepo ukabadilika baada ya Simba kumnyakua staa huyo na mashabiki wa timu hiyo, wakaanza kumpa ushujaa, huku wakiucheka upande wa pili.

Yanga haikukalia kimya usajili wake, ulipeleka kesi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo likampa haki Morrison, klabu hiyo ikakata rufaa Mahakama ya usuluhishi ya michezo (CAS) ambako nako kesi ikawashinda.

Pamoja na mikimiki aliyopitia, Gazeti la Mwanaspoti limekuchambulia mambo matano ambayo Morrison, yamemfanya aendelee kulinda heshima ya kipaji chake.

KUHIMILI MATATIZO

Alihimili kishindo cha zomeazomea ya mashabiki wa Yanga, wakati wa kusubiri majibu ya kesi ambayo ilikuwa Cas.

Hata hivyo halikuonekana ni jambo la kumtoa kwenye mstari wa kutimiza majukumu yake ipasavyo, ingawa hakuwa anaanza kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha aliyetimuliwa Didier Gomes.

KUTUNZA KIWANGO

Katika nyakati zake ngumu, aliendelea kukitunza kiwango chake, alionekana kuwa supa sabu, kwani alikuwa akipewa dakika kipindi cha pili, mara nyingi alibadilisha matokeo.

Alizidisha vituko nyakati ambazo alikuwa anataniwa zaidi, alivua bukta kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambayo Simba ilinyakua ubingwa Julai 25, mkoani Kigoma na wala hakuonyesha kujali.

NIDHAMU YA MAZOEZI

Pamoja na vituko anavyovionyesha nyakati mbalimbali, ana nidhamu ya mazoezi, yanayomfanya kuwajibika ipasavyo anapokabidhiwa majukumu na kocha wake.

SOMA NA HII  BERNARD MORRISON AKABIDHIWA TUZO YA MCHEZAJI BORA

Mwanaspoti limemshuhudia mara kadha mazoezini, Kocha akiwa anampa maelekezo ya nini afanye mara nyingi huku akiweka utani pembeni na kujituma zaidi.

KUTETEA KIPAJI CHAKE

Hajaishia kuridhika kuwa na kipaji pekee, bali anakitetea na kujituma licha ya jina lake kuwa kubwa na kupata wafuasi wanaopenda utendaji kazi wake.

MTAZAMO WAKE

Mtazamo wake ulionekana kuwa imara namna ya kuchukulia matatizo, hilo lilijidhihirisha wakati wa kesi yake, aliendeleza shughuli zake kama kawaida na baada ya kushinda alipata muda wa kuishukuru Yanga kumsajili kwa mara ya kwanza na kuacha mambo mengine kuendelea.

WADAU WAMPA DENI

Aliyekuwa beki wa Simba, Kasongo Athuman, anasema ni wakati wa Morrison kuonyesha kile ambacho mashabiki walikuwa wanakitamani kukiona kutoka kwake.

“Morrison yule aliyecheza dhidi ya Red Arrows mechi ya Caf ndiye alikuwa anasubiriwa na mashabiki, kesi imeisha, yupo huru ana deni na Wanasimba la kuwalipa kupitia mguu wake,” anasema.

Mtaalamu wa saikolojia Charles Nduki anasema inakuwa ngumu kwa binadamu kufanya kazi asilimia 100 endapo anakuwa na matatizo yanayomkabili.

“Hakuna kazi ngumu kama ya wanasoka, wanahitaji wataalamu wa saikolojia ili kuwajenga, mfano Morrison licha ya kwamba alikuwa anajitahidi kuonyesha furaha, ila asingeweza kuwajibika kwa asilimia 100,” anasema Nduki na anaongeza kuwa;

“Ndio maana kwa sasa anaonekana kiwango chake kipo juu zaidi, kwasababu akili yake inawaza kazi na yupo huru, sasa deni limebakia kwake kuwapa huduma nzuri Wanasimba.”