Home Makala PAMOJA NA YOOTEE…LAKINI UKWELI NI KUWA SABABU ZA BARBARA KUKASIRIKA NI HIZI...

PAMOJA NA YOOTEE…LAKINI UKWELI NI KUWA SABABU ZA BARBARA KUKASIRIKA NI HIZI HAPA…


JUMAMOSI iliyopita ilikuwa siku ya mechi ya watani katika Ligi Kuu Bara maarufu kama Kariakoo Derby iliyozikutanisha Simba na Yanga. Timu hizi zilitoka suluhu hali inayofanya mtaani kuwe shwari.

Katika hekaheka za mchezo wa watani wa jadi hapakosi matukio kadhaa ambayo mengine husababisha kutokea kwa mabishano katika mitandao na mitaani. Moja ya tukio ambalo nalo lilivuta hisia ni kitendo cha mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez kuzuiwa kuingia na watoto aliokuwa nao kupitia mlango wa VVIP.

Tukio hilo lilisambaa mitandaoni kupitia video fupi iliyokuwa inamwonyesha mwanamke aliyekuwa eneo la ukaguzi wa tiketi na mlango wa kuingilia akiongea na simu na huku katika ikisikika sauti ya Barbara akielezea tukio hilo.

Lakini, ongea yake haikuwa kama ambavyo amezoweleka kwa hali ya utulivu na upole, bali katika video hiyo alisikika akiongea kwa ukali huku pia akitumia maneno makali kuashiria kuwa alikuwa amekasirishwa.

Wahenga wanasema binadamu ana moyo wa nyama. Pale unapomuumiza hisia zake ni kawaida kuumia kihisia na kuzaa hasira au gadhabu.

Mara baada ya video hiyo kusambaa mitandaoni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo lilitoa tamko kuhusiana na tukio hilo. Ila swali la wengi ni kwanini hali ile ilimpata Barbara. Kwa jicho la kitabibu jibu ni rahisi ni kwa kuwa aliumizwa kihisia hali iliyomfanya kukasirika.

Hasira mara baada ya kuumizwa kihisia ndio sababu inayoweza kumfanya binadamu kupatwa na hali kama ile iliyompata Barbara. Uwepo wa hasira ni moja ya ishara za kimwili kujihami dhidi ya matukio mbalimbali yanayomkuta. Tukio la Barbara limenipa hamasa kutoa ufahamu kuhusu tatizo la hasira.

HIVI INATOKEAJE?

Hasira ni moja ya matokeo yanayoashiria kuwapo kwa hisia za kawaida. Lakini, hasira inapozidi mwilini mwa mtu ni jambo la hatari kiafya pamoja na mahusiano na kijamii. Hasira ya mtu inaweza kuwa ya kawaida, ya kati na ile kali iliyokithiri.

Chanzo cha hasira huwa ni matukio yanayomtokea mtu katika maisha ya kila siku. Yapo mambo ndani ya mwili kama vile kuwaza mawazo hasi na nje ya mwili kama vile kuudhiwa au kutishiwa. Uwepo wa hasira ni mwitiko wa kimwili kuonyesha hisia hasi za kimwili, huku kuwa na furaha huwa ni hisia chanya kimwili.

Hisia za kimwili huwapo katika eneo la maalumu kwenye ubongo. Binadamu hutumia hasira katika kujitunza na kujihami. Hasira huendelea kuwepo kwa mtu na kumtawala endapo atakuwa anaendelea kutumia hasira hiyo kama kielelezo cha maudhi aliyoyapata. Hasira huathiri uhusiano wa mtu kijamii, hisia za kimwili (kiakili) na kimwili. Mwilini mwetu Ubongo ndio wenye kazi ya kuratibu shughuli zote za mwilini. Kipo kituo maalumu ambacho kinahusika na hisia za kimwili.

Lakini, sehemu hiyo katika ubongo iitwayo Amygdala ambayo imo ndani ya mfumo uitwao limbic ndio inahusika na hisia za mwili. Sehemu hii hutambua uwepo wa hatari nje ya mwili, hivyo kuustua na kuupa tahadhari kuwa kuna tishio.

SOMA NA HII  UKWELI LAZIMA USEMWE...GOLI LA ORLANDO HALIKUWA HALALI...JE..VAR HAINA MSAADA KWA WAAMUZI..?

Sehemu hii ndio ya kwanza kugutuka kabla ya sehemu ya pili itwayo cortex ambayo hutafakari na kuhukumu mambo kama ni kujibu mapigo au kutulia wakati wa hatari. Sehemu hii ina sehemu ya upande wa kushoto yenye kazi ya kuzima sehemu inayohusika na hisia za mwili, hivyo hasira hudhibitiwa. Hii huwa ni baada ya kutafakari na kunyumbulisha matukio yaliyojitokeza.

MABADILIKO KIMWILI

Hasira kutokea hupitia hatua mbalimbali ndani ya mwili na akilini kwa ujumla. Hasira huambatana na utiririshwaji wa kemikali za kimwili pamoja na vichochezi (homoni) katika ubongo ambavyo husambaa sehemu mbalimbali katika mwili.

Vitu hivi kwa pamoja vinapotitirishwa huuufanya mwili kuwa na nguvu kuliko ilivyo kawaida ili kujihami kwa lolote. Mtu anaweza kupambana, kukimbia au kupoteza fahamu wakati tukio linapotokea. Na linaweza kuchukua dakika kadhaa kuwepo, baadae kama hasira itaendelea kuwepo basi mwili unaweza kutiririsha kiasi cha ziada cha kemikali na homoni za mfumo wa fahamu, na mwili kuweza kuanza kupambana.

Hatua hii huwa ya mwisho katika kuamsha hasira kali zaidi. Hivyo hapa mtu anakuwa katika hatua za kupambana vikali. Kemikali hizo na homoni zinapotiririka huambatana na mabadiliko ya kimwili na kiakili.

Mabadiliko huwa ni pamoja na mapigo ya moyo kushika kasi ili kulisha misuli damu ya kutosha. Mtu hupumua haraka haraka ili kuleta oksjeni nyingi zaidi. Mboni za macho na lenzi hutanuka kuweza kuona zaidi. Misuli huanza kujiweka imara na kuwa na nguvu.

Akili ya mtu mwenye hasira huwa makini zaidi kuliko kawaida na humlenga yule au kitu kilichomtisha na kumletea hasira. Ndio maana unaweza ukawa katika hatari kubwa ukaweza kuruka ukuta pasipo kutarajia na hapo baadaye ukajaribu kuruka ukuta huo pasipo uwepo wa hatari ukashindwa kufanya hivyo.

ATHARI KIAFYA

Uwepo wa hasira zisizodhibitiwa huwa na madhara kiafya, kimwili na kiakili. Madhara kama kuumwa kichwa, kukosa usingizi, kutokwa vipele, kukosa hamu ya kula, kuwa mwoga kupitiliza na mwili kuuma. Madhara mabaya zaidi ni kama vile kupata magonjwa ya moyo ikiwamo shambulizi la moyo (heart attack), sonona (depression) na shinikizo la kiakili.

Moja ya njia rahisi ya kukabiliana na hasira ili kupunguza ni kuongea kile kilichokusibu au kwa kuondoka katika eneo lililokupa maudhi au kukaa mbali na aliyekuudhi. Lakini, pia hata kwa kumweleza mtu mwingine jambo lililokuudhi au pale unapolisema kwa wengine kama alivyofanya Barbara ni sahihi ili kupunguza makali ya hasira.

Endapo utaona una hasira inayodumu na inayoshindikana kudhibitiwa fika katika huduma za afya, uwaone washauri nasaha au wanasaikolojia ama wataalamu wa afya ya akili.

Makala haya yameandikwa na Dr Shita Samweli na kuchapiswa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti