SIMBA inapiga hesabu za kumchukua kiungo wa Yanga Mukoko Tonombe taarifa hizo zimemfikia kocha wa vinara hao wa ligi Nesreddine Nabi akisema bado anamuhitaji mkongomani huyo.
Akizungumza hivi karibuni Kocha Nesreddine Nabi ametamka kwamba kikosi chake bado kinamuhitaji Mukoko na kwamba ameshatoa baraka zake katika mazungumzo ya kumwongezea mkataba.
Mkataba wa Mukoko na Yanga umebakiza miezi saba kumalizika ndani ya mwaka huu 2022 lakini uhakika ni kwamba Simba inapiga hesabu za kumchukua Mkongomani huyo.
Simba tayari imeshafanya mawasiliano kwa siri na Mukoko lakini kikwazo ni muda wa mkataba uliobaki kati ya Yanga na kiungo huyo ambapo wekundu hao wanajua mabosi wa Yanga hawataweza kukaa nao meza moja kumaliza dili hilo.
Nabi alisema anamuhutaji Mukoko aendelee kupigania nafasi katika timu yake.
“Mukoko sio mchezaji ambaye unaweza kumuachia kirahisi hasa hapa ndani, timu inamuhitaji bila kujali amekuwa akikosa nafasi ya kuanza mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita,” alisema Nabi ambaye leo ametua kwake Ubelgiji katika mapumziko mafupi.
“Mukoko anatakiwa kutuliza akili yake, kuna mambo yamekuwa yanalazimisha kukosa nafasi kwake ambayo ni suala la kanuni hizi za ligi za wachezaji nane wa kigeni kuanza katika mchezo mmoja.
“Lingine ni timu kuunganika, huwezi kubadilisha sana timu iliyo sawa sawa ili acheze lakini bado ana nafasi ya kuendelea kutuliza akili na kushindana na wenzake, huwezi kucheza na wachezaji walewale katika mashindano yote kuna wakati utakuja wakati mabadiliko yanahitajika, mpira uko hivyo.”
Aidha Nabi alisema haoni kama viongozi wa Yanga wanaweza kuruhusu Mukoko kwenda timu pinzani hapa na kwamba anaamini kiungo huyo ataongeza mkataba kama ambavyo amewataka viongozi kumbakiza.
“Nimewaambia viongozi wampe mkataba mpya kwangu nafasi anayo anachotakiwa kupambana sioni kama Yanga inaweza kukaa meza moja na Simba wakaongea kumuuza hapa ndani labda ingekuwa nje ya nchi hii sawa, lakini mpaka sasa hakuna ofa hiyo.”
NKANE MAPINDUZI
Winga Denisi Nkane ameungana na kambi ya timu yake mpya kwa ajili ya mashindano ya Mapinduzi akiwa chini ya kocha Cedrick Kaze.
Yanga imeondoka jana saa tisa mchana kwa boti ikiwakosa mastaa wao watano tu wa kikosi cha kwanza kutokana na kwenda kuyatumikia mataifa yao huku wengine wakiomba mapumziko.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema mastaa wao wote wanaondoka leo huku akimtaja winga wao mpya Nkane kuwa ameungana na timu na atakuwa miongoni m,wa wachezaji watakaoanza safari leo.