BAADA ya kukaa nje kwa muda mrefu mshambuliaji wa Simba, Chris Mugalu amefunguka kuwa amerudi na anaiona nafasi yake kikosi cha kwanza huku akimtaja straika wa Yanga, Fiston Mayele kuwa ni moja ya wachezaji tishio msimu huu.
Mugalu ambaye aliingia kambani mara 16 msimu uliopita alikuwa nje ya uwanja kwa muda kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja, ameweka wazi kuwa kurejea kwake ni chachu ya kuendeleza alipoishia.
Alisema akiwa nje ya uwanja hakuacha kufuatilia soka kwa sababu ndio mchezo anaoupenda na kukiri kuwa amevutiwa na upambanaji wa mshambuliaji wa Yanga, Mayele huku akimtaja Henock Inonga kuwa ni usajili bora uliofanywa na Simba.
“Mayele na Inonga niwachezaji niliofurahishwa na namna ya uchezaji wao. Wamekuwa bora zaidi kwenye michezo waliyocheza, navutiwa na uchezaji wao ni wapambanaji wana kila sifa za kuchezea timu hizo,” alisema.
“Kama wataendelea kuaminiwa na kupewa nafasi wataweza kuzisaidia timu Mayele anajua kucheza na akili za mabeki sio mviziaji kama washambuliaji wengine anatafuta na anafunga. Inonga ni beki mwenye akili ya mpira anatumia mguu na kichwa anaweza kuruka juu na pia ana jicho la kuona mshambuliaji anataka kufanya nini kwa wakati gani.”
Akizungumzia kurejea kwake alisema ameshuhudia ligi bora msimu huu ya ushindani, lakini hana hofu na chochote kwani anaamini katika kipaji chake na bado anaona anayo nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza Simba.
“Nimekaa nje kwa muda haina maana kwamba nimepoteza nilichonacho mguuni nina imani ya kufanya vizuri na natarajia kuwa miongoni mwa wachezaji watakao tetea taji la mara ya tano mfululizo timu ipo vizuri na tuna kila sababu ya kufanya hivyo,” alisema mchezaji huyo.
Mugalu alisema amefurahi kurudi ligi ikiwa bado mbichi na amekuta timu haijapumzika imeunga kushiriki kombe la Mapinduzi anaamini hilo ndio litampa nafasi ya kujiweka fiti kabla ajarudi kwenye ligi ya kushindania taji.