Timu ya Mbeya City imeendelea kujifua kujiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Simba baada ya kuisambaratisha Itezi FC mabao 4-1 huku ikishuhudiwa nyota wapya wawili beki, Hamadi Waziri na Kiungo wa zamani wa Wekundu, Shaban Kisiga wakiwa ndani.
Mbeya City Januari 17 Iitawakaribisha Simba mchezo utakaopigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa ukiwa wa raundi ya 12 kwa timu hizo.
Hata hivyo timu hizo zinakutana ambapo Mbeya City wanakumbuka kupoteza mechi mbili dhidi ya wapinzani hao walipokutana msimu uliopita, ambapo katika mechi ya nyumbani walifungwa bao 1-0, huku ya marudiano, City wakilala mabao 4-0.
Katika mechi ya leo ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa mazoezi uliopo mtaa wa Isyesye, Mbeya City ikiwa na kikosi chake na wachezaji Waziri aliyewahi kukipiga Ruvu Shooting na Kisiga walionesha ufundi mwingi na kupata ushindi huo.
Mabao katika mchezo huo, yamefungwa na Seleman Boban, Eliud Ambokile, Frank Ikobela na Juma Luizio, huku Kipa Deogratias Munish ‘Dida’ naye akionesha vitu safi kwa kuokoa michomo kadhaa langoni mwake.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mathias Lule amesema hawana wasiwasi na mchezo wao dhidi ya Simba na kwamba wanaiona mechi hiyo kama zilivyo nyingine.
Amesema anaamini mechi hiyo timu yake itapata matokeo mazuri, huku akieleza kuwa uwapo wa wachezaji, Kisiga na Waziri hawezi kuizungumzia kwani bado ni mapema japokuwa wapo kwenye mahesabu yake.
“Wachezaji kila mmoja ana ari naorari na ukizingatia inapofika mechi kama hizi za Simba, Yanga na Azam kila mmoja huonesha uwezo wake, hivyo ninaamini tutapata matokeo mazuri, kuhusu Kisiga na Waziri muda utaongea” amesema Lule.
Kwa upande wake Meneja wa timu hiyo, Mwagane Yeya amesema wachezaji hao wapo kwenye hatua za mwisho kumalizana na mabosi, huku akitaja majina ya nyota wanne ambao wamewatoa kwa mkopo.
“Wachezaji Babilas Chitembe, Edger, Mbembela, Issa Shaban na Methew Robert hawa tumewatoa kwa mkopo japokuwa tunasubiri uamuzi wao kama wamepata timu au tuwapeleke tulipopata, hivyo kufikia Ijumaa tutakuwa tumejua” amesema Yeya.