Wakati jana aliiongoza timu yake kupokea kichapo cha kwanza kutoka kwa Mbeya City, Kocha wa Simba, Pablo Franco amesema kuwa kwa upande wako anaona Azam FC wanayo nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa siku za mbeleni kutokana na kikosi chao kuimarika kila siku.
Pablo amesema amekutana na Azam FC kwenye mechi mbili kwa siku za hivi karibuni na ameona kuna utofauti mkubwa kwenye mechi ya kwanza na ya pili ambayo wamecheza na anaona kabisa timu ina ari ya kuwa bingwa.
Akizungumza na gazeti la Championi Jumatatu, Pablo alisema Azam wana kikosi bora na vijana ambao kwa siku za usoni wataifanya timu hiyo kuwa tishio na kuweza kutwaa ubingwa ambao wameukosa kwa muda mrefu sasa.
“Nimekutana na Azam kwenye michezo miwili kwa kipindi cha muda mfupi, nimeona wanabadilika na watakuja kuwa tishio na kuweza kutwaa ubingwa siku za usoni.
“Wana vijana wengi wenye vipaji na baada ya muda mfupi kila kitu kitakwenda sawa. Timu yao nzuri sana pengine kuliko watu wanavyofikiria,” alisema.
Simba walikutana na Azam FC, kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Kabla ya hapo walikutana kwenye ligi kuu na kuvuna ushindi wa 2-1