MMH! panafuka moshi. Mambo hayapo sawa kabisa kwenye ofisi za viongozi wa Manchester United kwa kile kinachoelezwa kwamba kocha Ralf Rangnick amekasirika juu ya viongozi hao kutosikiliza mahitaji yake ikiwa pamoja na mapendekezo ya wachezaji aliotaka wasajiliwe katika dirisha hili.
Mabosi wa Manchester United wamegoma kabisa kufanyia kazi mapendekezo ya wachezaji wanaohitajiwa na kocha huyo ambayo aliwasilisha mara tu baada ya kupewa timu mwezi Novemba mwaka jana.
Rangnick anadai kati ya makubaliano baina yake na mabosi wa Man United yalikuwa ni kumpa fungu la kusajili wachezaji kadhaa katika dirisha hili.
Pia katika makubaliano hayo mabosi wa Man United walimpa kocha huyo jukumu la kuhakikisha timu inamaliza katika nafasi nne za juu ili kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Mmoja kati ya watu wa karibu na kocha huyo amefichua kuwa Rangnick hana furaha na anahisi kama amefungwa mkono mmoja kwa sababu hapati kile anachohitaji.
Siku chache baada ya kuwasili, Rangnick alipendekeza aletewe kiungo wa RB Leipzig, Amadou Haidara ambaye Leipzig ilikuwa tayari kumuachia kwa Pauni 33 milioni tu lakini Man United ilishindwa kukamilisha dili hadi staa huyo akaondoka zake kuitumikia Mali kwenye michuano ya Afcon.
Vilevile mbali ya mashetani hao wekundu kushindwa kumsainisha Haidara kilichomuuma Rangnick ni kuwa staa huyo anatajwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutua Newcastle United ambayo tayari imeshaanzisha mazungumzo na wawakilishi wake.
Hiyo pia imemfanya kufikiria kuachana na timu hiyo ifikapo mwisho wa msimu huu licha ya kwamba atatakiwa kufanya kazi kama mshauri wa benchi la ufundi lakini yeye ameona kuna uwezekano mkubwa akaachana na kazi hiyo kwani mabosi sio wasikivu.
Kazi ya kwanza ya Rangnick ikiwa atabaki kwenye kikosi na kuitumikia miaka miwili kama mshauri wa benchi la ufundi itakuwa ni kusaidia kupatikana kwa kocha mpya kisha kuisaidia timu hiyo kwenye dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Rangnick mwenyewe alipowahi kuulizwa na waandishi kwenye moja ya mahojiano yake alisema: ”Nilijaribu kukaa vikao kadhaa na John Murtough, Ed na Richard kuhusiana na masuala ya usajili lakini mimi sio mtu mwenye uamuzi wa mwisho,” kauli hii iliendelea kuonyesha kweli kuna uwezekano mtaalamu huyo hapati anachohitaji.
Hata hivyo, wakati Rangnick anadhani kwamba kukosekana kwa baadhi ya wachezaji aliowapendekeza ndio imesababisha timu kutokuwa na matokeo mazuri, vyanzo vya kuaminika ndani ya Man United vimefichua kuwa wachezaji hawafurahishwi na mbinu zake kwani wanaona ni za kizamani.
Kwa sasa Man United inapambana kutafuta kocha mpya ambaye ataanza kuifundisha timu kwa msimu ujao na katika orodha yao kuna makocha kibao ikiwa pamoja na Mauricio Pochettino, Erik ten Hag na Brendan Rodgers lakini kocha anayepewa nafasi kubwa zaidi ni Pochettino kutokana na kuifahamu vizuri Ligi Kuu ya England akiwa amewahi kuzifundisha Tottenham na Southampton. Lakini kocha mwingine Ten Hag wa Ajax ambaye amependekezwa na Rangnick mwenyewe .