KUNA wachezaji wengi wanakuzwa na ukubwa wa majina ya Simba na Yanga. Wachezaji hao wanaishi kwa ujanjaujanja. Lakini, bahati mbaya ujanja huo haudumu sana.
Ndicho ambacho tunakiona kwa kiungo Said Ndemla. Mwanzoni mwa msimu Simba ilimtoa kwa mkopo kwenda Mtibwa Sugar. Simba waliamini timu yao imejaa mafundi wengi na Ndemla hatacheza. Ulikuwa ni uamuzi wa busara. Kwa miaka mingi wadau wa soka walikuwa wakipigia kelele jambo hilo. Walitaka Simba iwatoe baadhi ya wachezaji kwa mkopo kwenda timu nyingine ili wapate nafasi ya kucheza.
Ndio hao kina Ndemla. Wanakaa Simba mwaka mzima bila kucheza mechi hata tano za ushindani.
Msimu huu Simba ikaona isiwe tabu, ikamtoa kwenda Mtibwa Sugar. Na hapa ndipo tumeona uwezo halisi wa Ndemla. Kumbe ni mchezaji mzuri wa kawaida. Alikuwa akibebwa na upepo tu pale Simba.
Ndemla anacheza kwa uwezo wa kawaida Mtibwa Sugar. Muda mwingine anawekwa hadi benchi. Mchezaji unatokaje Simba ukakae benchi Mtibwa Sugar? Ni ajabu na kweli.
Pengine Ndemla alichelewa kuondoka Simba. Katika umri wake alitakiwa kucheza mechi nyingi za ushindani, lakini hakuzipata Simba. Benchi likawa linammaliza taratibu. Sasa amekwenda Mtibwa Sugar akawa mchezaji wa kawaida.
Kwa kiwango chake cha sasa, haonekani Ndemla akirejea tena Simba, labda kama ataongeza uwezo vinginevyo atasalia huko huko.