Home Azam FC AJIBU AMUA KUANIKA YOTE YALIYOMTOKEA SIMBA…AGUSIA SABABU YA KUIKATAA TP MAZEMBE..AITAJA YANGA…

AJIBU AMUA KUANIKA YOTE YALIYOMTOKEA SIMBA…AGUSIA SABABU YA KUIKATAA TP MAZEMBE..AITAJA YANGA…


KIUNGO mshambuliaji mwenye kipaji chake, Ibrahim Ajibu ‘Cadabra’ kwa sasa yupo Azam FC, ikiwa ni siku chache tu tangu maisha yamshinde Msimbazi.

Ndio. Uwepo wa ushindani mkubwa hasa nafasi yake, Ajibu alichoka kukaa benchi akafanya maamuzi magumu.

Uamuzi alioufanya hivi sasa sio kama ule alioufanya alipokwenda Yanga ambao ulionekana kama kuhusisha utani zaidi, lakini hivi sasa ni uamuzi ambao wengi hawakuutarajia hadi alipotangazwa.

Hakukuwa na tetesi zozote za kuondoka kwa Ajibu ndani ya Simba, ingawa mashabiki wengi walitaka na kutamani acheze hata timu nyingine ili kulinda kipaji chake, hapo ni namna gani utagundua kuwa mshambuliaji huyo ni kipenzi cha watu.

Ndani ya Simba msimu uliopita Ajibu alikuwa anawania namba na Clatous Chama na Luis Miquissone ambao walikuwa kikosi cha kwanza na msimu huu aliingia kwenye upinzani na nyota kama Hassan Dilunga, Rally Bwalya, Pape Ousmane Sakho, Peter Banda na Bernard Morrison.

Ajibu baada ya kumaliza mkataba wake pale Yanga arudi Simba, huku ikielezwa aliridishwa kwani ni mtoto wao na aliondoka kwa wema tu ili akajaribu changamoto mpya tofauti na baadhi ya wachezaji wengine wanaoondoka vibaya kwenye timu zao na hata sasa uongozi wa Simba umebariki kuondoka kwake ndio maana walimtakia heri katika maisha mapya.

Ajibu tayari amecheza mechi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi na kuonyesha kiwango bora kwamba akipambana zaidi, basi huenda akapata namba kikosini na kuisaidia Azam

Katika mahojiano na GAZETI la  Mwanaspoti yaliyofanyika visiwani hapa Ajibu anaeleza mambo mbalimbali juu ya soka lake kikubwa zaidi akisema anafurahia maisha mapya ndani ya Azam.

MAMBO BADO

Kwanza alizungumzia kuingia kwake ndani ya Azam ambayo haina mwendelezo mzuri kwenye ligi ingawa ni miongoni mwa timu bora na tajiri kwenye Ligi Kuu Bara kuwa ipo kwenye kipindi cha mpito.

“Haya ni matokeo tu ya timu hata Ulaya kuna timu kubwa na tajiri lakini hazina matokeo mazuri kwenye mechi, huwezi ukawa na mwendelezo mzuri wa moja kwa moja kwa miaka yote kuna wakati utatikisika.

“Naamini ligi bado ni mbicho kwa kushirikiana na wenzangu tutajitoa katika upambanaji ili kuipigania timu ianze sasa kupata matokeo mazuri na yenye kurejesha imani na matumaini kwa mashabiki wa Azam bado naamini inawezekana na muda upo,” anasema Ajibu.

NI SALAMA KWAKE

Anasema katika timu ambazo zipo salama kwake basi ni Azam FC. “Binafsi nipo sehemu sahihi na salama kabisa katika soka. Ni timu ambayo naona nimefanya uamuzi sahihi kwa sababu nitacheza na sio kukaa benchi.

“Nimetoka Simba ambako nilikuwa nakaa benchi kutokana na ushindani wa namba na sio kuwa kiwango changu kilishuka ama sina uwezo wa kucheza Simba, ila tumetofautiana na kila kocha ana mfumo wake na watu anaohitaji kuwatumia kwenye mfumo huo.

“Mchezaji anaweza kuonekana sio bora kwa mambo mengi, ushindani wa namba kuwa mkubwa ama kushindwa kuingia kwa haraka kwenye mfumo wa kocha ndio maana niliona ni vyema niondoke ili kulinda kipaji changu kwani soka ni kitu ninachokipenda.”

SOMA NA HII  KUELEKEA MSIMU UJAO..YANGA WAINGIA VITANI NA WAMOROCCO KUMWANIA GABADINHO..SENZO AANIKA KILA KITU...

HANA PRESHA

Ajibu anasema utulivu wa Azam FC kuanzia ndani ya uwanja na mashabiki tofauti na timu mbili alizochezea Simba na Yanga ambazo zina presha kubwa.

“Nadhani hakuna asiyefahamu presha za hizi timu Simba na Yanga. Zina presha kubwa kuanzia ndani hadi kwa mashabiki na ukiwa mchezaji wa kukata tamaa, basi huwezi kuishi muda mrefu kwenye hizo timu tofauti na hapa ambapo hawana presha kama hizo.

“Katika soka langu sijawahi kukatishwa tamaa na presha za mashabiki ama viongozi wa hizo timu kwani mara zote huwa nasimamia kile ninachokiamini ilimradi tu kiwe kitu sahihi na sio cha kukiuka maadili.

“Kwa ufupi ndani ya Azam najisikia kuwa na amani zaidi kwani wamenipokea vizuri kuanzia wachezaji hadi viongozi na ndio maana nimesema hapo awali kuwa tukiunganisha nguvu basi timu itatoka hapa ilipo na kuwa juu zaidi yote yanawezekana ila nipo mahali salama kabisa,” anasema Ajibu.

KUCHEZA NJE

Ajibu aliwahi kudaiwa kuwa alifuatwa na TP Mazembe ya DR Congo, lakini dili hilo alilipotezea ila bado anasema akipata nafasi ya kwenda nje kucheza ataenda, japo sio lazima sana kwake.

“Sasa wote tukienda kucheza nje nani atacheza hapa nyumbani? Kila mtu anatamani kucheza soka la kulipwa na hata mimi ikitokea basi nitaenda ila sio kihivyo isipotokea nitakuwepo hapa hapa na maisha yataenda tu,” anaeleza na kuonyesha kwamba hana haraka na soka la kulipwa.

TIMU YA TAIFA

Ajibu amewahi kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars mara kadhaa ingawa ni muda sasa, lakini yeye anaeleza namna anavyotamani kuichezea tena timu hiyo.

“Natamani kurudi Stars na ninaamini nitarudi kwani nilipo ni sehemu sahihi ya kunirejesha huko. Usahihi ni kwamba nitapata nafasi ya kucheza na kuonyesha ubora wangu.”

MIPANGO YAKE

Mchezaji huyo anasema kuwa msimu huu unaweza kuwa bora kwake ndani ya timu hiyo huku akiahidi kwamba akipata nafasi ya kucheza atafunga sana tu.

“Siwezi kusema nitafunga mabao mangapi, ila nikipata nafasi ya kucheza na nisipopata majeraha, basi nitafunga mengi tu ya kuwafurahisha mashabiki wa Azam na soka kwa ujumla. Naamini uwezo wangu,” anasema Ajibu anayekumbuka bao lake bora kabisa ni lile alilofunga kwa faulo akiwa Yanga.

USHAURI WAKE

Ajibu anawataka wachezaji wanaochipukia kupambana.

“Hata sisi hapa tulipofikia tumepambana sana, tumepitia changamoto nyingi hadi kufikia mafanikio kama haya.

“Sasa hivi kuna vijana wengi wanakuja kwa kasi nawasihi tu waongeze juhudi. Wasibwete katika kuyatafuta mafanikio naamini watafika mbali zaidi,” anasema.

KURUDI SIMBA

Nyota huyo anacheka baada ya kuulizwa swali iwapo kuna siku atatamani kurudi Simba, ambapo anajibu soka ndio kazi yake ila kwa sasa yupo Azam. “Kwa sababu bado sijafikiria kustaafu soka kutokana na umri wangu mdogo, basi siwezi kuzungumza zaidi kwa sasa kuwa nitarudi Simba ama la. Sasa mimi ni mali ya Azam na Simba ni timu iliyonilea na kunikuza kisoka, sijaondoka kwa ubaya. Acha nicheze mpira kikubwa ninachoshukuru ni kucheza timu zote kubwa za Ligi Kuu Bara.”