Home news WAKATI BARBARA AKISEMA HAWATAKI MAKOSA TENA….SIMBA WAMSHUSHA KIUNGO MNIGERIA DAR..

WAKATI BARBARA AKISEMA HAWATAKI MAKOSA TENA….SIMBA WAMSHUSHA KIUNGO MNIGERIA DAR..


MABOSI wa Simba wanapambana wakati huu kuhakikisha wanapata wachezaji wenye viwango bora na kuwasaini ili kuongeza makali ya kikosi chao, kilichotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku Kocha Mkuu Pablo Franco akilainishiwa mambo.

Simba usiku wa jana ilikuwa ikimalizana na Azam katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kisha Jumanne nyota wake watapanda boti kwenda visiwani Zanzibar kwa mechi za Kombe la Mapinduzi 2022 na ikitoka hapo moja kwa moja itasafiri kwenda Mbeya kwa mechi ya Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, ukiichungulia ratiba ya Ligi Kuu Bara kwa mwezi wa Januari ni wazi Simba ina unafuu flani kulinganisha na watani zao, Yanga na hata Azam ambao nao wakitoka katika Mapinduzi watasafiri ugenini kwa mechi za Ligi Kuu Bara.

Wakati Yanga ikitoka Mapinduzi itaifuata Coastal Union Januari 16, siku hiyo Simba itapepetana na Mbeya City na Azam itaumana na Mbeya Kwanza.

Ukiangalia timu zinazokutana na vigogo hao watatu ni wazi Simba na Azam zinamchekea, kwani hata mechi za kumalizia Januari, Simba itacheza na Mtibwa Sugar – Morogoro Januari 22, wakati Azam itakipiga na Tanzania Prisons – Sumbawanga na siku moja baadaye ni Yanga na Polisi TZ Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Kwa kuangalia rekodi ya timu hizo zinazokutana na vigogo ni wazi Kocha Pablo kalainishiwa mambo na kama vijana wake watakaza huenda wakaufurahia mwaka 2022, ingawa Yanga ya msimu huu inaonekana kuwa bora zaidi, lakini rekodi zao kwa wapinzani wake inawaangusha.

Msimu uliopita Coastal ilikuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga na Polisi ililazimisha sare ya 1-1 na kumfuta kazi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Cedric Kaze ambaye kwa sasa ni msaidizi wa Nasreddine Nabi.

Upande wa Simba, mechi na Mbeya City ugenini ilishinda 1-0 na ilitoka sare ya 1-1 na Mtibwa, ilhali Azam iliitungua Tanzania Prisons.

MNIGERIA AITWA DAR

Achana na ratiba hiyo, unaambiwa mabosi wa Simba wanahaha kushusha nyota mmoja wa kigeni kati ya wawili inayowapigia hesabu kabla dirisha dogo kufungwa, huku wakimuita kiungo Mnigeria Eop Udoh jijini Dar ikiendelea kumpigia hesabu Mkenya Harrison Mwenda anayekipiga Kabwe Warriors ya Zambia inayoitaka Msimbazi iwape hela kumuachia winga huyo mwenye mkataba.

SOMA NA HII  KARIA AIBWAGA SIMBA KAMA MASIHARA

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema inatafuta mchezaji mmoja wa kigeni wa kuziba nafasi ya Duncan Nyoni aliyevunjiwa mkataba.

Inaelezwa Simba imemtumia barua ya mwaliko Udoh ili kuja kucheza Kombe la Mapinduzi na kama atakuwa katika ubora watamsajili.

Udoh kwa sasa anaichezea timu ya Akwa United ya Nigeria iliyomsajili akitokea Arar FC iliyopo Ligi Kuu ya Saudia Arabia aliyojiunga nayo 2020 na ametumika katika mechi 13.

Mmoja wa mabosi wa Simba aliliambia Mwanaspoti wamemtumia barua ya mwaliko mchezaji huyo kuja kucheza Kombe la Mapinduzi, ili kama wakivutiwa naye wamchukue badala ya Mwendwa ambaye ishu ya mkataba wake ndio tatizo.

“Kama atakuwa mzuri vile tunahitaji tutakaa naye chini na kuona namna gani tunaweza kumpata lakini hilo litaamuliwa na kocha Pablo Franco kwani ndiye mwenye uamuzi wa mwisho,” alisema kigogo huyo aliyekataa kutajwa jina gazetini.

“Udoh anachosubiri ni tiketi ya ndege kutoka huko alipo ili kuja hapa kwa ajili ya kucheza Mapinduzi. Changamoto tuliyo nayo tuna nafasi moja ya kusajili mchezaji wa kigeni ndio huyo tunamtafuta. Ndio maana tupo makini kwelikweli kutafuta aliye sahihi kwa kuomba kuwaona, kushirikiana na wengine katika ushauri ili kukwepa kusajili vibaya kama dirisha kubwa.”

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema wapo kimya katika usajili kwani hawataki kurudia makosa.

“Bado hatujafanya uamuzi wa wachezaji wapya tutakaowasajili kwenye dirisha hili ndio maana tupo kimya tu ila tunao ambao tunawafuatilia na kabla ya dirisha kufungwa tutawaeleza hili,” alisema Barbara.