Home news PAMOJA NA SIMBA KUPITWA NA YANGA KWA POINT 10…PABLO AVUNJA UKIMYA …ATOA...

PAMOJA NA SIMBA KUPITWA NA YANGA KWA POINT 10…PABLO AVUNJA UKIMYA …ATOA KAULI HII…


KAMA ulikuwa unaamini Simba imesalimu amri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, basi pole yako, kwani wenyewe wamesisitiza bado wamo sana na hii inatokana na jeuri ya mechi zilizosalia kabla ya msimu haujamalizika.

Watetezi hao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 25 baada ya mechi 13 ikizidiwa pointi 10 na vinara Yanga wenye alama 35 kwa idadi sawa ya mechi na kuwafanya mashabiki wa Jangwani kuanza kuhesabu ubingwa.

Hata hivyo, kocha Pablo Franco licha ya kukiri pointi walizoachwa na watani wao ni nyingi na ni mara ya kwanza kwa historia kwa timu hizo zikiwa zimelinga michezo, lakini bado haiwaondoi Simba kuwepo kwenye mbio za ubingwa.

Pablo alisema, Simba haina presha na kelele za watani wao kuanza kujihesabia ubingwa, kwa vile ligi imesaliwa na mechi 17 ambazo ni nyingi kuliko zilizochezwa hadi sasa na anaamini watatetea ubingwa mwisho wa msimu.

“Hakuna aliyejua kama Simba ingecheza mechi tatu bila ushindi, vivyo hivyo hata kwa timu nyingine mambo yanaweza kutibuka, bado naamini tuna uwezo wa kuikuta na kuipita Yanga,” alisema na kuongeza;

“Katika michezo 17 tuliyobaki nayo kuna mmoja tutacheza nao (Yanga), hivyo hatuna presha na mashabiki na wapenzi wasikate tamaa, bado tuna nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wetu na kuweka rekodi.”

Pablo alisema hata hivyo anawaheshimu wapinzani wao wote wa Ligi Kuu na michuano ya ASFC, lakini kama timu wana malengo waliyojiwekea ikiwamo kutetea mataji yao na ndilo wanalolifikiria na kujipanga kutimiza hilo.

“Niwatoe hofu wanasimba, ni kweli kazi bado ni ngumu, kama benchi la ufundi hatutaacha kufanya kazi ya kutosha kutoa maelekezo na kuweka mipango sahihi katika kikosi chetu ili kuwa na matokeo mazuri katika michezo ijayo,” alisema.

Juu ya kupitwa pointi 10 alisema ni nyingi, lakini bado zinaweza kufikiwa kama watashinda mechi zao na wapinzani wao wakipata matokeo tofauti na waliyozoea.

“Kuwania ubingwa ni kama mbio za marathoni kuna wakati unaweza kuanza vibaya, njiani ukakutana na vikwazo, lakini mwishowe ukajipanga na ukamaliza kinara, hatuamini kama hatumo kwenye ubingwa. Subirini muone!”

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUFUNGIWA....KOCHA TAIFA STARS AIBUKA NA HILI TENA KUHUSU MOROCCO

Kwa misimu minne mfululizo iliyopita, Yanga ilikuwa ikiongoza msimamo kwa muda mrefu, lakini ikajikuta ikizidiwa ujanja mwishowe na Simba kutokana na misimu hiyo kuwa na mechi nyingi za viporo na pia Yanga kuwa na kikosi dhaifu.

Kwa msimu huu Yanga inaonekana kuwa na kikosi bora chenye wachezaji wenye viwango vya juu kulinganisha na wale wa Simba, lakini pia Bodi ya Ligi (TPLB) imepanga ratiba ambayo haitoi nafasi ya kuwepo kwa viporo vingi.