HII ni habari njema kwa mashabiki wa Simba, lakini huenda ikawa mbaya kwa wachezaji wanaocheza nafasi moja na kiungo Mganda, Taddeo Lwanga ambaye amerejea kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu.
Kiungo huyo mkabaji ameanza kufanya mazoezi mepesi akiwa amesaliwa na asilimia chache kabla ya kujumuika na wenzake kikosini.
Lwanga aliumia goti mwanzoni mwa msimu na ilisemekana angekaa nje ya uwanja kwa msimu mzima, lakini hali imeonekana kuwa tofauti.
Wakati anarudi Simba kwa sasa timu hiyo kiungo Sadio Kanoute yupo kwenye programu maalumu sambamba na Kibu Denis ambao juzi walikuwa kwenye mazoezi mengine ya peke yao.
Kiungo huyo alionekana akiwa sambamba na kocha wa viungo, Daniel De Castro ambaye alikuwa anamsimamia kuhakikisha anarejea kwenye makali yake.
Lwanga hakumuangusha kocha huyo kwani alikuwa anafanya kila zoezi la viungo ambalo alipewa na alionyesha utimamu wa mwili aliokuwa nao tangu mazoezi yanaanza mpaka yanamalizika.
Baadhi ya mashabiki waliokuwa katika Uwanja wa Mo Simba Arena walionekana kufurahishwa na urejeo wake baada ya kumuona akifanya mazoezi bila shida yoyote.
Kurejea kwa Lwanga kunafanya eneo la kiungo mkabaji Simba kuongezewa ushindani na kuwafanya wanaocheza nafasi hiyo yaani Jonas Mkude, Kanoute na Mzamiru Yassin kukaa mguu sawa. Pia kurejea kwake kumrahisishia kazi kocha Pablo Franco namna ya kuwatumia wachezaji hao.