Rais wa Heshima wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Wawakilishi pekee kwenye Michuano ya Barani Afrika Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ jana Jumatano (Februari 09)amezungumza na Wachezaji na Benchi la Ufundi la klabu hiyo.
‘Mo’ alifanya mazungumzo hayo kambini Jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya kuwatia hamasa wachezaji kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya Makundi dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Akizungumza na AZAM TV baada ya kikao na wachezaji na benchi la Ufundi, Mo amesema ameamua kufanya hivyo kwa lengo la kuonesha bado yupo pamoja na timu ya Simba SC, na bado anaipenda klabu hiyo , licha ya maneno ya mitandao kudai kuwa amejiondoa.
Amesema bado ana matumaini makubwa na Simba SC, licha ya kuteleza kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lakini uwepo wao kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho umewafanya kuendelea kujipanga ili waweze kufanya vizuri kimataifa msimu huu 2021/22.
Kama hiyo haitoshi, ‘Mo’ amesema hata upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara, napo wamejizatiti kuhakikisha wanatetea Ubingwa wao kwa mara ya tano mfululizo, licha ya kuanza vibaya kwa kupoteza michezo miwili na kutoka sare kwenye michezo minne.
“Nimewekeza kwenye klabu hii zaidi ya Bilioni 20, siwezi kuondoka Simba SC kwa sababu ninaipenda sana klabu hii tangu nikiwa mtoto,”
“Bado nipo Simba SC, tumekua kwenye klabu kumi bora za Barani Afrika na tumeonesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, mwaka huu tumeteleza na sasa tupo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini lazima tujipange kwa sababu haya ni mashindano yenye umuhimu mkubwa.”
“Bado tuna kazi kubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa hiyo lazima tuwe na malengo makubwa ili kufanikisha azma yetu na kuifanya Simba SC kuendelea kuwa kinara wa soka Tanzania.” Amesema Mo Dewji
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo wa kwanza wa Kundi D dhidi ya ASEC Mimosas Jumapili (Februari 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikipewa nafasi ya Mashabiki 35,000 watakaoshuhudia mchezo huo, utakaoanza majira ya saa kumi jioni.