KATIKA mitandao ya kijamii wiki iliyopita kuna hoja iliibuliwa na wadau kwa kulinganisha baadhi ya vitu vya sasa na vya zamani juu ya soka nchini ambayo ilionekana kuendelea kuwachukua muda mrefu kutokana na umuhimu wake.
Pia ni kutokana na ukweli wa pande zote mbili zinazokinzana.
Hoja yenyewe ilikuwa ni majina ya a.k.a ambazo mara nyingi wachezaji wa soka na hata wanamichezo wengine hupewa majina hayo na kusababisha majina wanayopewa kutokana na tasnia wanayoitumikia kujikuta ndio yanakuwa rasmi na yale majina yao rasmi kutofahamika kabisa katika jamii.
Katika mijadala ambayo mimi pia nilishiriki hasa kupitia mitandao ya kijamii, kwa mfano wadau walianza kusema kuwa majina ya a.k.a waliyokuwa wanapewa wachezaji wa zamani wa ndani ya nchi yanaonekana kuwa na taswira nzuri kuliko majina mbadala wanayopewa wachezaji wa sasa. Miongoni mwa mifano iliyotolewa katika mijadala ni jina kama vile Mwamba wa Lusaka au Tripple C ambalo huwa ndilo hutumika sana kwenye mijadala linalohusishwa na staa wa Simba, Mzambia Clatous Chama huku ukiangalia wachezaji wazawa majina wanayopewa hayana taswira nzuri kama vile nungunungu au kiungo punda.
Baada ya kuangalia mifano hiyo ikabidi nipitie majina mbadala ya wachezaji wa zamani wazawa waliyokuwa wakipewa – tena wahusika wakubwa wa kutoa majina hayo walikuwa ni watangazaji wa mechi husika ambazo wachezaji hushiriki na kusababisha watangazaji kutoa jina kiutani ambalo mara mara nyingi huendana na tukio au matukio ya mchezaji na kukuta jina hilo likitamalaki.
Kwa mfano, Sunday Manara aliitwa Kompyuta miaka ya 1970 wakati ambao hata kompyuta ilikuwa bado haijaanza kutumika nchini Tanzania au majina kama vile ya kina Godwin Aswile ambaye alipewa jina mbadala la Scania na kwa wakati ule lilikuwa ni kiashiria cha kubebea mizigo mizito, hivyo Aswile jina hilo liliendana na kazi yake.
Nakumbuka katika majina ambayo wachezaji wengine kipindi nikiwa nacheza walipewa majina ambayo yaliakisi kazi wanayoifanya uwanjani na majina hayo kuendelea nayo ingawa kuna majina mengine yalikuwa yanaonekana kama hayana taswira.
Nakumbuka tulikuwa na kina Steven Mapunda wakamwita jina la Garincha ambaye alikuwa mchezaji kutoka Brazil miaka hiyo aliyetambulika kama mchawi wa chenga. Halikadhalika Steven Mapunda alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kupiga chenga, Waziri Mahadhi walimwita Mendieta ambaye ni mchezaji wa zamani wa nchini Hispania.
Mlinzi Mohamed Abubakar ambaye aliitwa Phantom anbayo ilikuwa sinema ya kivita ya Kihindi iliyojaa mauaji ya kijeshi hivyo kutoa taswira halisi ya aina ya mpira aliokuwa akicheza akiwa CDA ya Dodoma na baadaye kucheza Yanga.
Mshambuliaji Joseph Kaniki aliitwa Golota kutokana na maumbile, lakini na aina ya soka kama mshambuliaji alivyokuwa akiupiga mwingi kipindi chake.
Madaraka Seleman walimwita Mzee wa Kiminyio kutokana na aina ya mpira aliokuwa akicheza ambapo kwa washambuliaji wengine ilikuwa ni kazi ngumu kupambana na walinzi wanaominya washambuliaji kwenye kugombania mpira, hasa mipira ya juu na ile mipira iliyokufa, lakini Madaraka alikuwa na uwezo wa kuminyana na walinzi.
Yapo mengine mengi tu kama vile kina Iddi Moshi aliitwa Mnyamwezi kwenye mechi ya Simba na Yanga ambapo alikuwa ametoka nyumbani kwao Tabora kufunga ndoa na aliporejea Dar es Salaam ndipo akacheza mechi hiyo na kufunga goli.
Katika mechi hiyo alipewa jina hilo mbadala huku Seleman Matola akipewa jina mbadala la Veron ambaye alikuwa ni kiungo wa soka kutoka nchini Argentina.
Naye Mwanamtwa Kihwelo alipewa jina la Dali KiMoko ambao ulikuwa muziki wa Zaire, hivyo jina hilo lilipatikana kutokana na aina ya ushangiliaji wa Mwanamtwa alipofunga.
Hivyo, ukiangalia aina ya majina mbadala waliyokuwa wakipewa wachezaji wa zamani mengi unaweza kuona kuwa ni majina ambayo yanafaa kuendelea kuishi nayo kutokana na umaarufu wa majina hayo kwa kulinganisha na majina halisi.
Lakini, kwa majina mbadala ambayo yanaonekana kutamalaki kwa wachezaji wazawa nadhani yanatakiwa kuangaliwa kwani ni vyema jina mbadala likawa na taswira nzuri ili hata pale mchezaji anapokuwa balozi wa biashara fulani inakuwa rahisi biashara hiyo kukubaliana naye kuliko jina likiwa na taswira hasi.
Hivyo kwa wanahabari na hasa watangazaji ni vyema tukaangalia aina ya majina mbadala kwa wachezaji wazawa kwani majina mbadala yana thamani kubwa sana sio tu uwanjani.
Ndio maana Bakari Malima hadi leo hii bado anaendelea kuwa Jembe Ulaya. Malima alikuwa fundi kwelikweli enzi zake akikipiga katika eneo la beki, ambapo timu pinzani zilikuwa zinakumbana na wakati mgumu kukabiliana naye anapokuwa akifanya vitu vyake uwanjani.
Ndio maana unajiuliza, inakuwa mchezaji aitwe nungunungu- jina la ajabuajabu?
Makala haya yaliandikwa na Ally Mayay na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti, mwandishi anapatikana kwa kupitia namba – 0658-376417