UNAAMBIWA huko mazoezini Yanga ni mwendo wa dozi tu kwani benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, lipo katika mipango ya kusuka ushindi katika mchezo unaofuata dhidi ya Biashara United unaotarajiwa kufanyika Februari 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mchezo huo ni wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports ambapo Yanga ilitinga katika hatua hiyo mara baada ya kuifunga Mbao FC kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Mayele.
Chanzo kutoka Yanga, kimesema kuwa, Kocha Nabi kwa siku za karibuni, ameongeza dozi kwa kufanya mazoezi mara mbili tofauti na awali ambapo walikuwa wakifanya mara moja.
“Kocha ni kama amechefukwa mara baada ya timu yake kupata sare katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, hivyo ambacho amekifanya ni kuongeza dozi ya mazoezi ndani ya timu ambapo kwa yanafanyika mara mbili tofauti na awali.
“Hapo awali mara nyingi timu ilikuwa ikifanya mazoezi mara moja na siku nyingine ndio ilikuwa mara mbili, lakini kwa sasa kila siku mazoezi ni mara mbili na hii ni kwa ajili ya kuipa timu ufiti kuelekea mchezo dhidi ya Biashara,” kilisema chanzo.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro, alisema: “Kila kitu kinakwenda vizuri ndani ya timu na matarajio yetu ni kuona timu inaendelea kufanya vema katika michuano yote ambayo tunashiriki msimu huu.”