YANGA ya msimu huu sio ya mchezo, kwani timu pinzani zikiamua kumkomalia nyota mmoja, basi wengine hasa wa kigeni wanawaadhibu na rekodi zinaonyesha kwa kikosi cha sasa ni Chico Ushindi tu na kipa Djigui Diarra ndio hawajatupia.
Katika msimu huu Yanga ina maproo 11, kati ya hao tisa tayari wameshafunga mabao kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), isipokuwa Ushindi aliyesajiliwa dirisha dogo na Diarra.
Mabao 23 ya Yanga katika Ligi Kuu, 17 yamefungwa na wageni huku sita yakifungwa na wazawa wakiongozwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’. Straika Fiston Mayele anaongoza akifunga sita, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ (4), Shaban Djuma (1), Tonombe Mukoko (1), Khalid Aucho (2) na Jesus Moloko (3). Nje na mabao ya ligi katika michuano ya ASFC straika wa timu hiyo, Heritier Makambo ana mabao matatu, huku Mayele akitupia mawili, ilhali kiungo Yannick Bangala juzi dhidi ya Biashara United alifunga bao moja.
Kwa upande wa wazawa waliofunga ni Fei Toto (4), Dickson Ambundo (1) na bao moja alijifunga Justine Bilary (Dodoma Jiji).
Mchambuzi wa soka George Ambangile alisema ndio maana halisi ya kikosi kipana kila mmoja anategemewa na wachezaji wenyewe wanatambua nini wanakifanya.
“Wanajenga kitu kimoja hawataki kugombea fito na ndio maana kila mmoja anapambana na akipata nafasi anafanya kile timu inatakiwa ifanye.Hamuwezi kuwa na matokeo mazuri kama kila mmoja anacheza ili aonekane yeye,” alisema.
Mchambuzi wa soka, Tigana Lukinja alisema kitu alichokitengeneza kocha Nasriddine Nabi ndani ya kikosi chake ndicho kimekuwa chachu ya mafanikio kwa wachezaji na sasa wanambeba.