HATUA ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu itaendelea leo Jumapili ikiwa inaingia raundi ya tatu ambayo itafunga dimba la mzunguko wa kwanza wa hatua hiyo.
Katika kundi D hadi sasa, wawakilishi wa Tanzania, Simba wanaongoza msimamo wa kundi hilo wakiwa na pointi nne walizokusanya katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Asec Mimosas na pia dhidi ya Gendarmerie Nationale.
Ilianza kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi nyumbani dhidi ya Asec ya Ivory Coast na baada ya hapo ikatoka sare ya bao 1-1 na Gendarmerie katika mechi iliyofuata ugenini huko Niger, Jumapili iliyopita.
Asec inashika nafasi ya pili kwenye kundi hilo ikiwa na pointi tatu sawa na RS Berkane lakini yenyewe ipo juu kwa vile imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara chache wakati huo Gendarmerie ikishika mkia na pointi yake moja.
Baada ya kukusanya pointi nne katika mechi hizo mbili za mwanzo, kibarua kinachofuata mbele ya Simba kwa sasa ni michezo miwili dhidi ya RS Berkane ambapo itaanzia ugenini huko Morocco, Jumapili mwishoni mwa wiki hii na baada ya hapo timu hizo zitarudiana hapa Dar es Salaam, Machi 13.
Kimahesabu, michezo hiyo miwili dhidi ya RS Berkane ugenini na nyumbani ndio itakuwa na nafasi kubwa ya kuamua nafasi ya Simba katika kundi D kama itasonga mbele au la kutokana na ratiba ya mechi za kundi hilo lilivyo.
Simba wanatakiwa kucheza mechi hizo mbili kama fainali na kuhakikisha inaibuka na ushindi katika michezo hiyo yote ambao utawafanya wafikishe jumla ya pointi 10 ambazo zitawafanya wajihakikishie tiketi ya robo fainali huku wakibakiwa na mechi mbili mkononi.
Kama wakishinda mechi hizo zote, maana yake RS Berkane na mojawapo kati ya Asec Mimosas na US Gendarmerie hazitoweza kufikisha pointi 10 hata kama zitashinda mechi mbili zitakazobakia kwani wakati Simba inakutana na timu ya Morocco, Gendarmerie na Asec Mimosas zitakutana zenyewe kwa zenyewe hivyo zitapunguzana pointi iwe kwa timu moja kufungwa au kutoka sare.
Kama itashindwa kabisa, Simba inapaswa angalau kupata pointi tatu au nne katika mechi hizo mbili ili iwe na uhakika wa kufikisha pointi 10 ambazo inaweza kuzipata kwa kushinda mojawapo kati ya mechi ya ugenini dhidi ya Asec Mimosas au ile ya kufungia dimba dhidi ya Gendarmerie nyumbani.
Lakini kama Simba ikipoteza mechi hizo mbili zinazofuata dhidi ya Berkane, ni wazi kwamba mambo yanaweza kuwa magumu kwao kwani watajikuta wakienda katika mechi mbili za mwisho huku wakiwa wamezidiwa kwa pointi tano na timu hiyo ya Morocco.
Na hali itakuwa mbaya zaidi iwapo Asec Mimosas nayo itashinda mechi mbili zinazofuata kwake dhidi ya Gendarmerie kwani nayo itawatangulia kwa pointi tano na bado itakuwa na faida ya kuwa na mechi moja nyumbani dhidi ya Simba.
Hali ikiwa kinyume na Gendarmerie ikaibuka na ushindi katika mechi zote dhidi ya Asec Mimosas, kimahesabu mambo bado yatakuwa magumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania.
Kimsingi, Simba hawapaswi kubweteka na pointi nne walizokusanya dhidi ya Asec Mimosas na Gendarmerie na wanatakiwa kupambana kwa machozi, jasho na damu katika mechi mbili dhidi ya Berkane.
Huu sio wakati kwao kujiamini kupitiliza na kuona kama wameshamaliza kazi kwani kwa kufanya hivyo watajikuta wakishindwa kujiandaa vizuri kimbinu, kiufundi na kisaikolojia kwa ajili ya mechi hizo na kuwapa mwanya wapinzani wao kuwaadhibu.
Wakumbuke kwamba kitendo cha kuongoza kundi bila kupoteza mchezo kinawafanya wapinzani kujiandaa vilivyo kwa ajili ya kukabiliana nao jambo litakaloongeza ugumu kwenye mechi zao zaidi ya ule ziliokutana nao katika michezo ya nyuma.
Kuongoza kundi sio tiketi kwa Simba kuingia robo fainali na badala yake ili lengo la kucheza hatua hiyo litimie wanatakiwa kukusanya pointi za kutosha ambazo hazitaweza kufikiwa na timu mbili kati ya tatu zilizopo kwenye kundi lake.
Siku zote shujaa ni yule anayecheka na kutabasamu mwisho baada ya kufanikisha kutimiza malengo aliyojiwekea.
Hakutokuwa na maana yoyote kwa Simba kuongoza kundi kwa sasa halafu baadaye washindwe kufuzu hatua ya robo fainali.
Wasiruhusu kufungwa na Berkane katika mechi mbili zijazo ili wafunge hesabu mapema na kuanza kujiandaa na robo fainali.