Mwenyekiti wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ismail Aden Rage ameibuka na kuweka wazi hali wanayoipitia katika kipindi hiki katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanznaia Bara.
Kabla ya mchezo wa juzi Alhamis (Februari 03) Simba SC ilikua haijapata ushindi kwenye michezo mitatu mfululizo dhidi ya Mbeya City, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, huku ikiambulia alama moja.
Rage amesema kinachoikuta Simba SC katika kipindi hiki cha msimu wa 2021/22 ni jambo la kawaida, na anaamini ni sehemu ya mchezo wa soka ambayo huitokea klabu yoyote duniani.
“Haiwezekani mkashiriki kwenye mashindano yenye timu 16 halafu ukataka wewe pekeyako kila siku ushinde hakuna Ligi ya namna hiyo”
“Mkitaka ushindi wa namna hiyo basi unatakiwa wewe uanzishe Ligi yako unakuwa na Simba A, B ,C,D E mpaka F ambapo kila mkicheza basi kila siku Simba lazima itashinda” amesema Rage alipozungumza kwenye kipindi cha Kipenga ya East Africa Radio.
Simba SC ilirejea kwenye njia ya ushindi juzi Alhamis (Februari 03) kwa kuifunga Tanzania Prisons 1-0, kwa mkwaju wa Penati uliopigwa na Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere.
Ushindi huo umeiwezesha Simba SC kufikisha alama 28, zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Young Africans ikiwa kileleni ikiwa na alama 35.