Home news WAKATI WATU WAKIFURAHI KIWANGO CHA BOCCO..MWAMEJA AMTAZAMA WEEE..KISHA AKAFUNGUKA HAYA…

WAKATI WATU WAKIFURAHI KIWANGO CHA BOCCO..MWAMEJA AMTAZAMA WEEE..KISHA AKAFUNGUKA HAYA…


LICHA ya baadhi ya mashabiki wa soka kumtazama kwa jicho la kushuka kiwango nahodha na straika wa Simba, John Bocco, lakini nahodha wa zamani wa timu hiyo, Mohammed Mwameja ameshauri nyota huyo kupatiwa huduma ya kisaikolojia ili kuwa sawa.

Hata hivyo, Bocco ambaye amekuwa akishtumiwa kwa kutofunga mabao katika siku za karibuni, kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas alisaidia upatikanaji wa mabao mawili kati ya matatu iliyopata Simba katika ushindi wa mabao 3-1.

Wakati Bocco akianza kurejea taratibu katika anga zake, Mwameja amekwenda mbali zaidi na kusisitiza kuwa ni miongoni mwa washambuliaji watatu bora kwake na hajachuja kama ambavyo baadhi ya mashabiki wamekuwa wakifikiria.

“Namuona Bocco kama mshambuliaji namba moja Tanzania bila ubishi kwa washambuliaji wetu wazawa. Kwenye tatu bora hakosekani hiki anachopitia sasa ni upepo na huwa inamtokea mchezaji yeyote,” alisema katika mahojiano maalumu na  gazeti la Mwanaspoti.

Alisema kinachomkuta Bocco sasa ni kuwa kwenye mwendelezo tofauti na ni kipindi cha mpito ambacho ili kukiepuka tiba yake ni kupata mtaalamu wa saikolojia.

“Ana kiwango bora. Hajachuja na bado anaweza kuwa tegemeo kwenye kikosi cha Simba kama atapata mtu wa saikolojia kumuweka sawa na maneno ya nje ya uwanja hasa yale ya kukatisha tamaa asikubali yakae kwenye akili.”

Japo hivi karibuni Bocco hakutaka kuzungumzia kipindi hiki anachopitia, Mwameja alisema anapaswa kukichukulia kuwa ni cha mpito, atulie na akianza kufunga atafunga hadi watu watashangaa.

“Soka la Tanzania lina makocha makocha wengi. Wapo wenye fani lakini pia lina makocha wasio na fani, hivyo ukiwasikiliza wote wanakuvuruga,” alisema.

Kuhusu safari ya ubingwa msimu huu, Mwameja alisema mbali na Yanga na Simba pia kuna Azam na Mbeya City zinapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu.

“Ubora wa kikosi cha Yanga msimu huu nafasi iliyopo kwenye msimamo ni dhahiri inampa presha Simba kutetea ubingwa, lakini tusiziangalie hizo timu mbili tu kuna Azam na Mbeya City zinakuja vizuri.

SOMA NA HII  TETESI....MANZOKI KUONEKANA KWENYE SIKU YA WANANCHI YA YANGA....MIPANGO YOTE NI KIMYA KIMYA NAMNA HII...

“Tangu Azam wamebadili kocha kuna mabadiliko. Hivyo lolote linaweza kutokea aliyetarajiwa kuwa bingwa au mshindi wa pili ikawa tofauti,” alisema.

Yanga ina pointi 36, Simba 31, Azam ni ya tatu na pointi 24 ilhali Mbeya City ina pointi 23. Simba pekee ndio imemaliza mechi za raundi ya kwanza lakini nyingine zimesalia na mechi moja kila moja.

“Hapo ukiteleza tu maana yake umeachwa. Nauona mzunguko wa pili utakuwa ni wa kufa na kupona,” alisema.