UONGOZI wa Simba SC, umefunguka na kuwatoa hofu mashabiki wake na kuelezea kurejea kikosini kwa kipa wao namba moja, Aishi Manula.
Manula hakuwepo kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United ambapo Simba ilipata ushindi wa mabao 3-0 kwenye Dimba la Benjamini Mkapa, Dar, Ijumaa iliyopita.
Katika mchezo huo ambao golini alikuwa Beno Kakolanya, Manula alikosekana kwa kuwa na matatizo ya kifamilia, lakini sasa amerejea na anatarajiwa leo Jumatatu kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji itakayochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amefunguka kuwa: “Manula amesharejea kikosini na kuanza mazoezi na wenzake, kwa hiyo ni jukumu la kocha kumtumia au la katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji.
“Kwa sasa hali ya kikosi ipo vizuri na kila mchezaji ana morali na mchezo huo, ukiangalia mchezo uliopita tulishinda kwa kishindo, hivyo wachezaji wanajiamini sana na wana hamu na mchezo huo.
“Tukimaliza mchezo na Dodoma Jiji, wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja na baadaye watarejea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.”
Akizungumzia mchezo wa leo ambao utaanza saa 1:00 jioni, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, alisema: “Hatujafanya mazoezi muda mrefu maana ni siku moja na nusu tu, tunahitaji kufanya vizuri ili kuwapa furaha mashabiki wetu.
“Nilitamani kupata muda mrefu wa kufanya mazoezi na wachezaji wangu ila ndiyo hivyo tuna muda mfupi na kwa sasa tunafanya mazoezi tofauti ili kupata matokeo mazuri.
“Napenda sana jinsi wachezaji wangu wanavyojitoa kutokana na mazingira.“Kesho (leo) mtaweza kuona sura mpya ambazo ni muda mrefu hazikuonekana uwanjani, atakosekana Kapombe ambaye aliumia mchezo uliopita na wachezaji wengine walioumia.”
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Mohamed Muya, alisema: “Tangu tumemaliza mchezo na Ruvu Shooting tuliweka kambi kwa ajili ya mchezo na Simba japo ni muda mfupi tangu tuchukue timu.
“Wachezaji wengi wapo salama na utimamu wa mwili, tutawakosa wachezaji watano ambao wengine ni majeruhi na wengine wana adhabu.