RASMI Kocha Mrundi Masoud Djuma atakaa katika benchi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya Kwanza kesho kutwa kufuatia uongozi wa timu ya Dodoma Jiji kutangaza kupata vibali vya Mwalimu huyo kufanya kazi nchini.
Djuma alishindwa kukaa katika benchi la timu hiyo katika michezo miwili dhidi ya Ruvu Shooting na Simba kutokana na kutokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.
Hivi karibuni Dodoma Jiji ilitangaza kuachana na Mbwana Makata na nafasi yake kuchukuliwa na Djuma na kocha msaidizi Muhammed Muya ambaye amechukua nafasi ya Renatus Shija.
Akizungumza Jijini Dodoma Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Fortunatus John amesema anafurahi wameweza kupata vibali vya kufanya kazi vya Mwalimu huyo.
Amesema kesho kutwa atakaa katika benchi katika mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Aidha Mtendaji huyo amesema wamesaini kandarasi na kocha huyo hadi mwisho wa msimu na kama timu itafanya vizuri watamwongezea mkataba.
“Makubaliano yetu atusaidie tumalize katika nafasi ya nne, lakini furaha yetu ni morali ambayo ameiongeza katika timu pia anataka timu icheze na hii ndio falsaha yetu,” amesema Fortunatus.
Kwa upande wake Djuma amesema atapambana kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri katika michezo yake.