YANGA juzi ililazimishwa sare ya ya kufungana bao 1-1 na timu ya taifa ya Somalia katika mchezo wa hisani wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku mabosi wa timu hiyo wakiweka wazi hawatazuia mchezaji yeyote kuuzwa kama atakuwa anahitajika.
Uongozi umesema kitu muhimu ni taratibu za kununuliwa kwa mchezaji husika zizingatiwe, ila ukweli milango yao ipo wazi kwa yeyote kwani wataleta majembe mengine ya maana ya kuifanya Yanga iendelee kuwa imara na tishio zaidi. Kauli hiyo imekuja baada ya kuenea tetesi kwamba straika Fiston Mayele anatakiwa na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, japo mtendaji mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa alishakanusha kuwa hakuna ofa yoyote kwao kutoka Sauzi na kwingineno.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hersi Said alisema hakuna mchezaji atakayezibiwa riziki kama atatakiwa na timu ya nje au klabu nyingine ya ndani ilimradi taratibu zifuatwe.
Hersi alisema mpira wa sasa umebadilika na unahitaji mtu atoke ili kutoa nafasi kwa wengine kuingia na kutoa mfano kwamba walikuwa na kina Simon Msuva, Tuisila Kisinda na mastaa wengine, lakini wote walitolewa na wengine kusajiliwa.
“Hatuwezi kuwabania wachezaji hata kidogo. Yeyote ataka-yepata nafasi ya kutoka tutamuachia atoke akajaribu maisha kwingine. Mpira siku hizi ni zaidi ya ajira,” alisema Hersi na kufafanua kuwa walimuuza Kisinda kwenda RS Berkane kwa kuvuna Dola 150,000 ilihali wao walimnunua kwa Dopla 30,000, hivyo kwa muda mfupi walinufaika naye kwani fedha zake zimewaleta nyota wengine klabuni hapo.
“Kupitia mauzo yake mchezaji huyo mmoja tuliwanunua mastaa watatu Djuma Shaban, Fiston Mayele na Jesus Moloko wote wanafanya vizuri,” alisema Hersi.
Nyota hao watatu kwa pamoja wamefunga jumla ya mabao 14 mbali na asisti zao kikosini.
Pia, Hersi alizungumzia kikosi cha Yanga akisema licha ya kuwa na majeruhi wengi kikosini, lakini bado haiwazuii kufikia malengo yao ya msimu huu ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
“Msimu huu tumejipanga kuhakikisha tunachukua ubingwa kuwa na majeruhi ni sehemu tu ya mchezo. Tuna kikosi kipana wachezaji wote wana uwezo mkubwa na ndio maana akiumia mmoja mwingine ataziba nafasi yake,” alisema.
Yanga ndio inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 45 baada ya mechi 17, ikifunga mabao 29 na kufungwa manne, huku ikiwa ni moja ya timu zilizotinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ikitarajiwa kuvaana na Geita Gold mwezi ujao.
Timu hiyo juzi ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Somalia, huku nyota wao mpya, Chico Ushindi aliyesajiliwa kutoka TP Mazembe ya DR Congo akibadilishwa na Mukoko Tonombe alifunga bao la kusawazisha dakika ya 25 akimalizia krosi ya Djuma Shaban.