Home Habari za michezo KUHUSU ISHU YA MASTAA YANGA KUPEWA MIKATABA MIFUPI…INJINI HERSI AFUNGUKA HAYA…

KUHUSU ISHU YA MASTAA YANGA KUPEWA MIKATABA MIFUPI…INJINI HERSI AFUNGUKA HAYA…


UONGOZI wa klabu ya Yanga umefichua sababu za kuwasajili wachezaji kwa mikataba mifupi ni kutokana na mifumo ya soka hapa nchini ilivyo.

Klabu nyingi za Tanzania zimekuwa na utaratibu wa kuwapa wachezaji wake mikataba mifupi ikiwemo miezi sita, mwaka mmoja hadi miwili na Yanga wameweka wazi sababu ya wao kufanya hivyo ingawa hawakutaja idadi ya wachezaji wenye mikataba ya namna hiyo.

Mwenyekiti kamati ya usajili ya Yanga, Hersi Said alisema moja ya sababu kubwa ni aina ya skauti inayofanyika kuwapata wachezaji hao na asilimia kubwa wanasajiliwa bila kuwafahamu kiundani tangu akiwa chipukizi zaidi ya kuwaona wiki kadhaa tu.

“Ni ngumu sana kumfanyia skauti mchezaji hapa nchini kuanzia alipoanza mpaka ukubwani kutokana na aina ya mifumo ya upatikanaji wao ilivyokuwa, sasa kama shida iko hapo unawezaje kumsajili mchezaji kwa mkataba wa muda mrefu halafu akiharibu gharama tu za kuvunja nae mkataba sio mchezo, itakulazimu kumtumia hivyo hivyo hata kama kiwango kimeshuka,” alisema Hersi.

Hersi alisema hiyo ndiyo sababu inayowafanya kutoa mikataba mifupi tofauti kwa ajili ya maslahi ya timu na mchezaji husika.

“Halafu hizi timu hazina pesa ya kufanya sajili ndefu, mchezaji ukimfuatilia toka chini na kujua mwenendo wake unaweza kumpa mkataba mrefu lakini ni elimu ambayo inatakiwa kutolewa kwa watu maana wengine wanalalamika tu huyu mchezaji mzuri mkataba kapewa mfupi kwa sababu hawajui,” alisema Hersi.

Inafahamika kuwa wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu ni Bakary Mwamnyeto, Farid Mussa, Zawadi Mauya, Yassin Mustafa, Kibwana Shomari, Deus Kaseke, Yacouba Sogne na Saido Ntibazonkiza.

Kuhusu nyota wao ambao mikataba inaelekea ukingoni alisema, hakuna mchezaji mzuri ambaye watakubali kumuachia aondoke bali watawaongeza mikataba kutokana na mahitaji ya kocha wao Nasreddine Nabi.

SOMA NA HII  VIDEO: YANGA KUSUKA UPYA KIKOSI CHAKE,