MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amesema hakuna wa kuizuia Simba kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika,lakini akajilipua kwa kutaja mechi nne za kuitoa Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Rage amesisitiza Yanga kukaa kileleni kwa msimamo hakuwezi kuinyima Simba ubingwa msimu huu na ana uhakika kutokana rekodi na kiwango cha Mnyama.
“Yanga wataanza kupotea dhidi ya KMC, Azam FC, Simba na Mbeya City wataambulia sare tayari mnyama atakuwa ametetea taji lake mara ya tano mfululizo hilo lipo wazi kutokana na timu hiyo kuwa wanyonge wa timu nilizozitaja pamoja na kupata matokeo mzunguko wa kwanza,” alisema Rage mwenye uzoefu na soka la Tanzania na Afrika.
Rage ambaye ana uelewa mkubwa wa sheria na kanuni za soka, aliongeza, ndani ya misimu minne ambayo Simba imetwaa mataji Yanga imekuwa ikiongoza ligi baadae inaishia kutazama taji likienda Msimbazi.
Yanga ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hadi sasa huku ikiongoza msimamo wa pointi 45. Simba ni ya pili ikiwa na pointi 37 lakini imeshapoteza mechi mbili huku Namungo ikipoteza nne na Azam sita.
ROBO FAINALI CAF
“Simba ni timu ya kimataifa, kazi yao kubadili ndege angani, nina uhakika na hilo, kikubwa wachezaji wafanye wanachostahili chini ya maelekezo ya kocha wao,” alisema na kuongeza,
“Hii ni nafasi ya Simba kupambania taji la Afrika, wanaweza kufanikisha hilo, kwani kundi lao lipo wazi, kwanza wana uzoefu na hilo wanachotakiwa ni umakini mkubwa.”
Naye kiraka wa Simba, Erasto Nyoni amewapongeza wachezaji wenzake; “Umoja ndio kila kitu maana wachezaji wote kwa umoja walipambana na kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wa Berkane, pia kufanyia kazi kile ambacho mwalimu alitaka kifanyiwe kazi.”