KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi amefichua siri ya timu hiyo kwa msimu huu kulinganisha misimu miwili iliyopita akisema kutumia kwake staili ya kocha maarufu duniani, Jose Mourinho ya kutumia wachezaji walio tayari kushindana.
Mourinho aliyepo AS Roma ya Italia hupenda kusajili wachezaji walio kamili katika kuingia uwanjani na kumpa matokeo tofauti na staili aliyokuwa akiitumia Arsene Wenger ya kuchukua wachezaji chipukizi ili kuendelea kuwakuza polepole.
Sasa staili hiyo ndiyo aliyotumia Nabi katika madirisha mawili ya usajili ya msimu huu, akisema ndio yameifanya Yanga kuwa tishio na kuonyesha upinzani wa kweli tofauti na ilivyokuwa misimu mitatu nyuma.
Nabi alisema misimu mitatu iliyopita Yanga ilikuwa inasajili wachezaji wengine si wa kuingia katika kikosi cha kwanza na walikuwa wanashindwa kutumika mara kwa mara kwa sababu mbalimbali.
Alisema msimu huu wachezaji wengi aliowasajili walikuwa kwenye ligi shindani tena wanatumika, wazaoefu na mambo mengine ya kiufundi ndio maana amewachukua na wamefanya kazi iliyokuwa anahitaji kutoka kwao.
“Ukiamuangalia Mourinho ndio mwenye tabia hiyo anapenda kuchukua wale wachezaji wengi wenye uzoefu na kuweza kushindana na wakampa matokeo ndani ya muda mfupi,” alisema Nabi na kuongeza;
“Katika kikosi changu kuna wachezaji wapya asilimia 80, wenye sifa nyingi za namna hiyo na tunaona kwa kiasi gani wamekuja kuongeza ubora wa kikosi chetu pengine tofauti na misimu iliyopita,”
“Ukiangalia Yanga ya msimu huu mbali ya wachezaji wenye uzoefu na waliocheza kwa ushindani huko walipotoka tumeongeza nguvu kwa kusajili wengine vijana kama, Denis Nkane, Aboutwalib Mshery, Crispin Ngushu, Yusuph Athumani ambao naamini nao katika siku zijazo watakuwa msahada na kutumika zaidi.”
Katika hatua nyingine Nabi alisema amefanikiwa kwenye usajili wa msimu huu madirisha yote mawili kutokana na muda aliyokuwepo katika timu ni tofauti kabisa na makocha wengine waliopita hivi karibuni.
Nabi alisema alichukuliwa na Yanga msimu uliopita ligi ikiwa inaendelea alipata kuona wachezaji wengi aliokuwa anawahitaji katika maeneo mbalimbali na wengi kati ya hao wamesajiliwa na wachache waliwakosa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Alisema makocha wengine waliopita hawakupata muda wa kutosha kama ambavyo ilikuwa kwake kwani mbali ya kusajili alipata muda wa kwenda kufanya nao maandalizi ya msimu ingawa haukuwa wa kutosha.
“Usajili wa msimu huu nieleze ukweli nawashukuru viongozi wa Yanga wamenisikiliza zaidi mahitaji yangu ya kiufundi na kusajili wachezaji niliokuwa nikiwahitaji na siyo vingine,” alisema Nabi.
“Nina imani kwenye usajili mwingine hatutaongeza wachezaji wengi kama ilivyokuwa msimu huu, ila tutasajili wachache na wale wenye tija ili kuongeza makali ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao.”