UONGOZI wa Simba, umepanga kuliandikia barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuomba waongezewe idadi ya mashabiki kutoka ile ya awali walioruhusiwa ambayo ni mashabiki 35,000.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi D dhidi ya US Gendarmerie utakaopigwa Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema wapo katika hatua za mwisho za kuandika barua watakayoipeleka CAF kuomba kuruhusiwa kuingiza idadi kubwa zaidi ya mashabiki ambayo wanaamini itajibiwa vizuri.
“Malengo yetu yalikuwa ni kufuzu hatua ya robo fainali kwa kuwafunga ASEC, lakini imekuwa tofauti.
“Hivyo katika mchezo wetu dhidi ya Gendarmerie, nguvu tunazielekeza kuhakikisha tunapata matokeo mazuri hapa nyumbani.
“Katika kuhakikisha tunaongeza hamasa na hali ya kujituma kwa wachezaji wetu, tumepanga kuwaandikia barua CAF kuomba waturuhusu kuongeza idadi ya mashabiki kutoka ile ya sasa,” alisema Ally.