MAKIPA tofauti wa Ligi Kuu Bara, wamekiri kipa wa Simba, Aishi Manula amewafunika kutokana na kiwango alichoonyesha dhidi ya Asec Memosas ya Ivory Coast Mnyama alivyolala mabao 3-0.
Kitendo cha Manula kuokoa penalti mbili katika mchezo huo, angalau kimewapa nguvu mashabiki wa Simba kutembea kibabe mtaani, huku wakiweka matumaini dhidi ya USGN ya Niger ili kupata nafasi ya kutinga robo fainali ya CAF.
Wanaocheza nafasi hiyo, wamezungumzia ukomavu wa Manula kwenye michuano ya CAF na namna anavyojiwekea heshima ya namna yake Afrika.
Kipa wa Ruvu Shooting, Mohamed Makaka alisema anachokifanya Manula kinamuonyesha namna alivyokomaa kudaka mechi za kimataifa na kujitengenezea heshima Afrika.
“Anazidi kutangaza kiwango chake Afrika, kudaka penalti mbili kwenye mchezo mmoja siyo kazi rahisi, kwa ujumla Simba ipo vizuri kimataifa ni fursa kwa wachezaji kutanua upatikanaji wa ajira nje,” alisema.
Kipa wa Mbeya City, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema; “Manula anadhihirisha uwezo wake kimataifa, ikumbukwe anakutana na wachezaji wenye viwango tofauti na vile vilivyozoeleka Ligi Kuu Bara ni jambo zuri kupata changamoto tofauti itakayomfanya afanye vyema hadi kwenye ligi ya ndani.”
Kipa mstafu Steven Nemes, aliyewahi kuzitumikia Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Majimaji ya Songea, alisema mabeki walimuangusha Manula hawakujitoa asilimia mia kukaba na wakati mwingine walikuwa wanagongana wenyewe kwa wenyewe.
“Manula akiendelea kujitoa hivyo, ataandika rekodi ya aina yake Afrika itakayokuwa inampa heshima, wakitajwa makipa wazuri kwenye michuano ya CAF naye atatajwa kwa kile anachokionyesha.” alisema.
Kocha wa makipa wa Mbeya City, Ally Mustapha ‘Barthez’ alisema: “Anajua kuutumia vyema wakati alionao, akiendelea kukaza ndivyo anavyozidi kujitengenezea heshima yake kwenye michuano hiyo, mfano alivyoacha alama ya kukumbukwa kwa wale ambao amedaka penalti zao.”
Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Ivo Mapunda alisema: “Manula anaonyesha ukomavu wa hali ya juu kwenye michuano hiyo, mabao aliyofungwa ni udhaifu wa timu nzima, ila uwezo wake binafsi umeonekana, ninachoweza kumshauri aendelee kufanya mazoezi zaidi yatakayomsaidia.”