KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa kwa sasa mawazo yao yote yapo katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam na wala hawauwazii mchezo wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba utakaopigwa Aprili 30, mwaka huu.
Yanga ambao ni vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 48 walizokusanya katika michezo 18, watakuwa ugenini kuvaana na Azam, Azam Complex, Dar es Salaam, Aprili 6, mwaka huu.
Akizungumza kocha Nabi alisema: “Tunajua tuna michezo migumu sana mbele yetu dhidi ya Azam kisha Simba, michezo hii miwili bila shaka itatoa mwanga wa ni wapi tutakuwa tunasimama katika vita ya kushinda ubingwa msimu huu.
“Lakini sisi kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla mawazo yetu yote kwa sasa ni juu ya kuhakikisha tunashinda mchezo dhidi ya Azam kabla ya kuanza kufikiria kuhusu mchezo wa dabi dhidi ya Simba.”