Home news AKIWA NA STAILI YAKE YA KUSHANGAILIA KWA KUTETEMA….MAYELE AWATISHIA ‘NYAU’ SIMBA…

AKIWA NA STAILI YAKE YA KUSHANGAILIA KWA KUTETEMA….MAYELE AWATISHIA ‘NYAU’ SIMBA…


HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba kufikia mchezo ujao dhidi ya KMC Machi 19 wachezaji wao wengi majeruhi watakuwa wamepona kabisa huku straika Fiston Mayele akiwatisha Simba akisema amedhamiria kuweka rekodi kwa kuzifunga timu zote 15 zinazoshiriki Ligi Kuu katika msimu wake wa kwanza nchini.

Mayele ndiye kinara wa kutupia kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 10 sawa na straika wa Namungo, Reliants Lusajo, lakini staa huyo wa Yanga ametoa pia asisti tatu tofauti na Lusajo mwenye asisti mbili.

Kufikia sasa, Mayele aliyetambulishwa kujiunga na klabu hiyo ya Wananchi Julai 31 mwaka jana baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, ameshazifunga timu tisa zinazoshiriki Ligi Kuu na hivyo amebakisha timu sita kutimiza ndoto yake.

Timu ambazo zinaugulia maumivu ya Mayele kwenye ligi ni Biashara United ya Mara, Dodoma Jiji, Mbeya Kwanza, Coastal Union, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam FC, KMC na Geita Gold ambao amewafunga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba juzi Jumapili.

Kagera Sugar ndio timu pekee ambayo iliifunga mabao mawili kwenye ligi tofauti na nyingine ambazo amezifunga bao moja-moja.

Mtihani uliopo mbele yake ni dhidi ya Namungo, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, Mbeya City, Tanzania Prisons na Simba ambayo kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii aliifunga bao lililoamua mchezo, lakini kwenye duru la kwanza la Ligi hakuweza kutikisha nyavu wanamsimbazi kwani mechi hiyo ilimalizika kwa suluhu.

Akilizungumzia hilo, Mayele alisema: “Natamani kufunga kwenye kila mchezo kama mshambuliaji ili kuisaidia timu kufikia lengo, malengo yetu ni makubwa, hilo linanifanya kuwa na njaa zaidi ya mabao, nakumbana na ushindani mkali ila huwa najitahidi kwa kufanya kazi ya ziada ili kufunga.

“Hakuna mchezaji ambaye hapendi kuweka rekodi, nitafurahi kuzifunga timu zote, lakini furaha kubwa zaidi kwangu itakuwa kutwaa ubingwa, bado kuna kazi kubwa mbele yetu, hiki ni kipindi ambacho tunatakiwa kuongeza nguvu.”

Baada ya michezo miwili ijayo ya ligi kwa Yanga ambayo ni dhidi ya KMC na Azam, Mayele atafukuzia rekodi Aprili 30 na Mei 4 ambapo chama lake litakuwa na mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba na Maafande wa Ruvu Shooting.

SOMA NA HII  KONKONI:- TAARIFA ZANGU KUHUSU YANGA ZINA NIA MBAYA....

Kama akiweza kutetema kwenye michezo hiyo, Mayele atakuwa na deni kwenye michezo mingine miwili mfululizo ambayo itafuata dhidi ya Namungo, Mei 8 na Prisons, Mei 15 huku michezo dhidi ya Polisi Tanzania na Mbeya City ambazo nazo hajazifunga, itachezwa Juni 11 na 12.

MAJERUHI

Wachezaji ambao wanasumbuliwa na majeraha ni Fiston Mayele, Crispin Ngushi, Yacouba Sogne, Jesus Moloko, Bryson David, Khalid Aucho, Farid Mussa na Saido Ntibazonkiza.

“Tuna idadi kubwa ya majeruhi na tunakamiwa sana, tunaomba wachezaji walindwe, mfano mchezo wa jana (juzi) mchezaji mmoja anafanya madhambi mawili ndani ya dakika tatu lakini anapewa kadi ya njano hii sio sawa kabisa,” alisema Nabi.

“Tuna siku nyingi za maandalizi ya mchezo dhidi ya KMC kwahiyo tunawapa mapumziko kisha wakirejea tutacheza mechi ambayo tutaangalia utimamu wa mwili wale ambao walikuwa majeruhi na wale ambao walikuwa hawajapata muda wa kucheza.”

MASTAA WAFUNGUKA

Wakati timu ikiwasili jana kutokea Mwanza, mastaa wengine wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Crispin Ngushi walikuwa wamekuja uwanja wa ndege na ndipo mastaa hao nao kwa kifupi walifungka kuhusu hali zao za afya mpaka sasa.

Ninja alisema; “Mimi niliumia sawa na Kibwana (Shomari) na nipo fiti kama yeye, siku zote nilikuwa nafanya mazoezi.”

Upande wa Ngushi alisema: “Naendelea vizuri kabisa, nitarudi kukipiga.”