Home Habari za michezo BAADA YA KUKIANDAA KIKOSI CHAKE DHIDI YA USGN….PABLO KAJISHIKA KIUNO…KISHA AKASEMA HAYA…

BAADA YA KUKIANDAA KIKOSI CHAKE DHIDI YA USGN….PABLO KAJISHIKA KIUNO…KISHA AKASEMA HAYA…


WAKATI US Gendarmerie ya Niger wakitarajia kutua nchini leo tayari kwa mechi ya kuhitimisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco ameahidi mashabiki wao mambo mawili; kushinda na kuonyesha kandanda safi katika mchezo huo utakaopigwa Jumapili wiki hii.

Katika mchezo huo utakaopigwa saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba yenye alama saba sawa na RS Berkane ya Morocco, inahitaji ushindi ili kutinga robo fainali ya michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa barani humu.

Katika Kundi D, ambalo linaundwa na Simba, Gendarmerie, RS Berkane, Asec Mimosas ya Ivory Coast watakaokuwa ugenini nchini Morocco Jumapili, ndio vinara wakiwa na alama tisa, hivyo sare tu inawatosha kutinga robo fainali.

 Pablo alisema kwa sasa hawana cha kufikiria zaidi ya mambo mawili, kushinda, lakini pia kuwapa burudani mashabiki wa Simba.

Alisema anaamini wachezaji wake watafuata kile alichowaelekeza na kuwapa furaha mashabiki, lakini la muhimu zaidi kwao ni kusaka ushindi ili kufikia malengo yao ya kufuzu robo fainali.

“Lengo la kwanza kubwa ni kuhakikisha tunashinda mchezo huo ambao ni fainali kwetu, pia kuonyesha kandada safi la kuvutia mashabiki watakaojitokeza kutusapoti siku hiyo,” alisema.

“Tunajua tunahitaji kushinda ili kuwapa furaha mashabiki, naamini watajitokeza kwa wingi, jukumu letu benchi la ufundi na wachezaji ni kuhakikisha tunawapa furaha ikiwamo kushinda mchezo huo.”

Kuhusu hofu ya Simba kumkosa kiungo wao mshambuliaji, Pape Sakho, taarifa kutoka Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, kinachoongozwa na Ahmed Ally, zimeeleza alipata maumivu ya mguu katika harakati za kuwania mpira mazoezini kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, lakini kwa sasa yupo fiti na jana alitarajiwa kuendelea na mazoezi.

“Daktari amewatoa hofu mashabiki wetu, Sakho hakupata majeraha makubwa anaendelea vizuri na leo (jana atarejea mazoezini na atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani Jumapili kuikabili Us Gendarmerie,” alisema Ahmed Ally.

SOMA NA HII  BAADA YA KUTIMULIWA KIMYA KIMYA YANGA...ZAHERA ALA SHAVU POLISI TZ...

Wakati huo huo, jana Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, alizindua kampeni ya hamasa kwa mashabiki kuelekea mchezo huo.

Katika uzinduzi huo, uliofanyika Stendi ya Mabasi ya Magufuli Mbezi, Dar es Salaam, Mangungu alisema uongozi pamoja na wachezaji wote wapo imara kuelekea kwenye mchezo huo na yeye binafsi akiahidi kununua tiketi 200 na kuzigawa kwa mashabiki ili kwenda kuisapoti timu Jumapili.

Kuhusu taarifa ya baadhi ya wachezaji wao kumaliza mikataba, Mangungu alisema: “Kuna baadhi ya watu ambao wanazungumzia kumalizika kwa mikataba ya wachezaji wetu wakidai wanataka kuwasajili kamwe hawatafanikiwa kwa sababu tunafahamu hizo ni propaganda tu,” alisema.

Katika uzinduzi huo, ulihudhuriwa na matawi 26, jambo ambalo uongozi wa klabu hiyo umewataka hata kuzidi kuhamasishana kuhudhuria uwanjani siku hiyo ili kushirikiana pamoja kufanikisha ushindi kwa kuwasapoti wachezaji.