Home Uncategorized KABENDERA ASHINDWA KUPUMUA, WAKILI AIANGUKIA MAHAKAMA

KABENDERA ASHINDWA KUPUMUA, WAKILI AIANGUKIA MAHAKAMA


Upande wa utetezi katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili mwandishi wa habari za uchunguzi Erick Kabendera umeiomba mahakama kuliamurau Jeshi la Magereza kumpeleka mshtakiwa huyo hospitali yoyote ya serikali ikiwamo Muhimbili kupata vipimo kwani anasumbuliwa na maradhi yasiyojulikana kwani hawezi kupumua wala kutembea sababu amepooza mguu.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai hayo leo Agosti 30,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega wakati kesi ilipokuja kwa ajili ya kutajwa baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile aliyepangiwa  kusikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.

Wakili Kambole amedai, mteja wao anasumbuliwa na maradhi yasiyojulikana ikiwamo kupoteza nguvu mwilini, kushindwa kupumua vizuri wakati wa usiku na kuzimia mara kwa mara.

Mapema, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa lakini kuna maeneo bado wanaendelea na uchunguzi kwa hiyo upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa utetezi, Kambole alidai kuwa wanaomba Jamhuri kuharakisha upelelezi kwa sababu mshtakiwa anakabiliwa na tuhuma ambazo hazina dhamana na pia mshtakiwa ana matatizo ya afya tangu usiku wa kuamkia Agosti 21, mwaka huu akiwa gerezani alianza kuumwa mpaka leo bado hali yake haijaimarika anapata shida kupumua inapofika usiku.

“Mheshimiwa mimi mwenyewe nilikwenda kumwona mshtakiwa, anashindwa kutembea anaishiwa nguvu na wakati mwingine anapoteza fahamu (kuzimia), mpaka sasa ndugu zake hawafahamu kinachomsumbua ni nini hivyotunaomba mahakama itoe amri kwa Jeshi la Magereza kumpeleka mshtakiwa hospitali yoyote ya serikali ikiwamo Muhimbili kwa ajili ya kupata vipimo vinavyostahili ili apate matibabu na ijulikane anaumwa nini, mshtakiwa ana haki ya kupata huduma bora. ” amedai Kambole.

Akijibu hoja hizo, Wankyo alidai kuwa atafikisha taarifa mahali husika kuhusu kuharakisha upelelezi na pia kuhusu matibabu jeshi la magereza lina utaratibu wake wa kutoa huduma za matibabu kwa watuhumiwa.

“Si sahihi mahakama hii kutoa amri kulielekeza jeshi hilo kwamba apelekwe hospitali gani kwa sababu hajasema kama amekosa huduma hiyo gerezani, tuhuma zinazomkabili mshtakiwa zinasikilizwa na Mahakama kuu kwa hiyo mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza hoja na kutoa uamuzi”alidai Wankyo.

Akifafanua zaidi Wankyo alidai kuwa kama utetezi wana hoja wawasilishe mbele ya Hakimu anayesikiliza usikilizwaji wa awali wa kesi hii.

Hakimu Mtega amesema amesikiliza hoja za pande zote mbili, amezihifadhi mpaka hakimu anayehusika na jalada hilo atakaporudi,  mshtakiwa arudishwe mahabusu mpaka Septemba 2, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kabendera anadaiwa katika siku tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Pia anadaiwa kushindwa kulipa kodi ya sh. 173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe TRA huku pia anadaiwa kujipatia Sh. Milioni 173.2 wakati akijua kuwa fedha hizo ni za kutakatisha na zao la makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

SOMA NA HII  KELVIN YONDANI AHUSISHWA SIMBA