Home Makala BAADA YA KUPITA MIAKA MINGI…MASOUD DJUMA AFUNGUKA A-Z NAMNA ‘UCHEBE’ ALIVYOMTIMUA SIMBA…

BAADA YA KUPITA MIAKA MINGI…MASOUD DJUMA AFUNGUKA A-Z NAMNA ‘UCHEBE’ ALIVYOMTIMUA SIMBA…


UONGOZI wa Dodoma Jiji umempa mkataba wa miezi sita kocha wao mpya Mrundi, Masoud Djuma ambaye atakuwa hapo kwa muda huo na lengo la kwanza ni kuhakikisha ‘Walima Zabibu’ hao hawashuku.

Kama Djuma atafanikisha kuibakisha timu hiyo kwenye ligi msimu ujao na kusalia katika ligi tena katika nafasi za juu mkataba wake utaongezwa mwaka mmoja kwani watakuwa wamelizika nae.

Gazeti la Mwanaspoti lililofanya mahojiano maalumu na Djuma linafahamu katika mkataba huo kuna kipengele kinaeleza kabla ya kufanya uamuzi wa kwenda kokote baada ya kumaliza muda wake Dodoma Jiji ndio wa kwanza kupewa nafasi.

Djuma ambaye atakiongoza kikosi cha Dodoma Jiji kwa mara ya kwanza Jumapili ya wiki hii katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ugenini amefunguka mambo mengi katika mahojiano haya ikiwemo suala la kuondoka Simba.

MAISHA YA SIMBA

Mwishoni mwa mwaka 2018, Djuma aliondoka katika kikosi cha Simba baada ya kusitishiwa mkataba wake kutokana na mambo mengi yaliyoelezwa wakati huo ikiwemo kushindwa kuelewana na kocha mkuu, Patrick Aussems.

Djuma anasema akiwa katika kikosi cha Simba alifanya kazi na makocha wawili wa kwanza, Joseph Omong na Pierre Lechantre na hapakuwa na shida aina yoyote ndani ya timu hiyo.

Anasema ila baada ya kuja, Patrick Aussems hata kwa upande wake alikuwa anashangaa kusikia kuna shida kati yake na Mbelgiji huyo ambaye alikuwa akimpatia ushirikiano wote ndani na nje ya kazi.

“Kuna nyakati nilishindwa hata kuelewa timu ilikwenda kucheza nje ya Dar es Salaam lakini hakutaka kusafiri na mimi na hapakuwa na sababu ya msingi ambayo alieleza,” anasema Djuma na kuongeza;

“Baada ya kuona hivyo na utulivu kati yetu haukuwa tena kama awali nilimfuata Aussems na kumuuliza shida ilikuwa nini hakutaka kusema na mwisho wa siku niliitwa ofisini kuambiwa mkataba wangu umesitishwa,”

“Niliuliza shida ni jambo gani nikambiwa tu ni maamuzi ya kocha mkuu basi sikutaka kuwa na mengi zaidi nilifanya maamuzi ya kurudi kwetu tena baada ya Simba kunipatia stahiki zangu zote.”

KWANINI ALIWATEKA MASHABIKI?

Djuma anasema kabla ya kuja Simba huko kwao Rwanda alikuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka kutokana na kazi yake ambavyo alikuwa anafanya akiwa kiwanjani pamoja na kuishi nao vizuri nje ya uwanja.

Anasema hata baada ya kuja Tanzania alikuwa na utamaduni huo nje ya uwanja aliishi vizuri na mashabiki wa Simba ikiwemo kuwepo katika shuhuli za kijamii zile za nje ya uwanja.

“Nikiwa uwanjani nilikuwa natengeneza kikosi ambacho naamini kitakwenda kuwapa furaha mashabiki wa Simba ila kingine ni baraka tu kutoka kwa Mungu ndio maana kila ninapokwenda kufundisha lazima mashabiki watanipenda,” anasema Djuma na kuongeza;

“Umeona hata hapa Dodoma nikuhakikishie nitakuwa kipenzi cha mashabiki kwa muda wote nitakao kuwepo.”

FAMILIA BONGO

Kulikuwa na taarifa katika maeneo mbalimbali kwamba Djuma wakati anaondoka hapa nchini kulikuwa na familia yake nyingine ameiacha na baada ya kurudi kwao hakuwa anaitunza.

“Kwanza nashangaa sijui zile taarifa zilitoka kwa nani kwamba nimeacha familia yangu hapa baada ya kwenda kutafuta maisha mengine katika nchi mbalimbali nilizopita baada ya kuondoka Tanzania,” anasema Djuma na kuongeza;

“Naomba leo niweke wazi hapa watu wangu wote ambao nilikuwa nao karibu kushirikiana katika kila jambo la ndani na muhimu kwa maisha yangu niliendelea kuwasiliana nao,”

“Si kuwasiliana nao bali kuisha katika kila shida na raha kwa akila ambaye nilikuwa nae karibu hapa nchini na hata wakati huu nimerudi tena nitaendelea kuwa nao kama hapo awali.

BAADA YA KUONDOKA SIMBA

Djuma anasema hakuondoka Simba katika mazingira mazuri kwani hata kiakili hakuwa sawa wakati ule kutokana na baadhi ya maratajio yake hakuwa ameyafikisha.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE - FARIDI MUSSA KAPELEKA KESI NGUMU YANGA...WAKIZUBAA SIMBA WANAMBEBA...

Anasema kuna malengo mengi alijiwekea kuyafikia Simba machache kati ya hayo aliyafikia ila yale mengine alishindwa tena kutokana na sababu za mtu mwingine kwahiyo hakuwa vizuri wakati ule.

“Nilirudi nyumbani kwanza kupumzika kwani kwa muda niliokuwa Simba maisha yangu kwa kiasi kikubwa yalibadilika kutokana na kile ambacho nilikuwa napata kutoka kwao kwa nyakati tofauti,” anasema Djuma na kuongeza;

“Baada ya kupumzika kama miezi sita hizi nilikwenda DR Congo kuna timu fulani nilifundisha kule lakini ilikuwa kwa muda wa miezi sita ila kushindwa kwao kunilipa stahiki zangu niliachana nao,”

“Nilirudi nyumbani nikaamua kwenda kusoma na kuongeza taalamu yangu hii ya ukocha pamoja na mambo mengine ili kuongeza weledi katika soka ambalo kila siku linabadilika.

“Baada ya hapo nilifanya kazi Burundi na timu ya mwisho kuifundisha kabla ya kuja hapa ilikuwa Rayon Sports ya Rwanda niliyoshindwana nayo kutokana na mambo fulani hivi binafsi.”

COASTAL, POLISI TANZANIA WAANZA

Djuma anasema kabla ya kufanya maamuzi ya kujiunga na Dodoma Jiji alianza kupokea simu za watu tofauti kutoka Polisi Tanzania na Coastal Union zilizoonyesha nia ya kumuhitaji.

Anasema awali aliongea na kiongozi wa Polisi ila walishindwa kukubaliana kutokana na mambo fulani ya kimaslahi na akashindwa kuja Tanzania kujiunga nao.

“Siku chache kabla ya kukubaliana na Dodoma Jiji, Coastal Union nao walikuwa wamewasiliana nami kuona jinsi gani wanaweza kunipata kwani nahisi walikuwa katika mchakato wa kuachana na kocha wao,” anasema Djuma na kuongeza;

KUTUA DODOMA

Djuma anasema baada ya majaribio mbalimbali ya timu kutoka Tanzania na nchini nyingine alikubaliana na Dodoma kutokana na mipango ambayo walimueleza na wanaamini chini yake inawezekana.

Anasema viongozi tofauti wa juu Dodoma waliongea vizuri masuala ya msingi kama maslahi, malengo ya timu, kuboresha kikosi, ushirikiano kutoka kwao pamoja na mengineyo.

“Baada ya kuona mambo mengi ya msingi kutoka kwao tumekubaliana nikafanya tu maamuzi ya kujiunga nayo huku nikiachana na ofa nyingine kutoka timu nne tofauti kutoka Kenya na Uganda,” anasema Djuma na kuongeza;

“Maamuzi haya ya kutua Dodoma niliwasiliana na watu wangu wa karibu kutoka Tanzania ambao siku zote nimekuwa karibu nao na walinieleza ni moja ya kikosi chenye wachezaji bora na naweza kufikia mafanikio.”

MALENGO DODOMA

Djuma anasema kabla ya kufanya maamuzi ya kujiunga na Dodoma aliuliza viongozi wa timu hiyo malengo yao ni yapi na aliambiwa jambo la kwanza timu ibaki kwenye ligi msimu ujao na kama atafanya vizuri zaidi ataongezwa mkataba wa mwaka mmoja.

Anasema kabla ya kuwapa majibu aliwasiliana na watu wake wa karibu wenye uweledi wa soka la Tanzania kuhusu timu hiyo na jambo hilo linawezekana na wote walimpa majibu mazuri. “Baada ya hapo nikaunganisha na vile vilivyo katika akili yangu kutokana na kuifuatilia ligi pamoja na Dodoma nikaamini hilo la kufanya vizuri na kuibakisha linawezekana kwahiyo nilikubaliana nao,” anasema Djuma na kuongeza;

“Mambo ya utambulisho wangu yalipo kamilika nilikwenda mazoezi kabla ya kuanza kazi niliwambia wachezaji kile ambacho kipo mbele yetu na kila mmoja anatakiwa kupambana ili kutimiza majukumu yake,”

“Nataka kila mchezaji kucheza kwa moyo wote katika kila mechi na kubadilisha mambo fulani ya kiufundi kwani kikosi hichi kina wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kucheza vile nahitaji katika falsafa zangu.

“Viongozi nao nimewaeleza nahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwao katika mambo yote ya msingi tena kwa wakati na baada ya muda mfupi kikosi cha Dodoma kitakuwa na mabadiliko makubwa katika uchezaji na matokeo mengi ya ushindi mzunguko huu wa pili.”

Makala haya yaliandikwa na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti.