Home Habari za michezo BAADA YA SIMBA KUCHAPWA JUZI…BARBARA KAONA ISIWE TABU AISEE..KAANIKA YOTE ALIYOFANYA PABLO…

BAADA YA SIMBA KUCHAPWA JUZI…BARBARA KAONA ISIWE TABU AISEE..KAANIKA YOTE ALIYOFANYA PABLO…


Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amesema kwa jinsi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco alivyoibadilisha Simba na kuitengenezea hali ya ushindani, anaona kabisa wakienda kutimiza ndoto zao za kutetea mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, sambamba na kutikisa Afrika ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Jumapili (Machi 20) Simba SC ilifumuliwa mabao 3-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast mjini Cotonou, Benin katika mchezo wa kusaka nafasi ya kutinga Robo Fainali kabla ya kurejea nchini kuisubiri USGN ya Niger kukamilisha michezo ya Kundi D la michuano ya Shirikisho.

Licha ya kipigo hicho, mapema Barbara alisema Simba SC imekuwa na mabadiliko makubwa tangu iwe chini ya Kocha Pablo waliyemuajiri Novemba mwaka jana baada ya kuachana na Kocha Didier Gomes na kusema mabadiliko hayo yameonekana wazi katika michezo inayocheza timu hiyo katika Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Amesema kikosi chao kimekuwa na mabadiliko makubwa kiufundi kwani mbali ya kushinda michezo mingi, pia kimekuwa kikicheza soka la kuvutia muda mwingi, kitu ambacho mwanzoni mwa msimu hali haikuwa hivyo na kuwakera mashabiki wa timu hiyo.

Amesema pia Pablo amerudisha nidhamu na morali kwa wachezaji wa Simba kucheza kwa damu zaidi na kila mmoja kutamani kuona timu hiyo inafikia mafanikio kwenye kila mashindano na kwamba wapinzani wao kwa sasa lazima wakae kwa akili kwani wakizubaa watapata tabu sana.

“Unajua unaweza kukuta viongozi tunawapatia kila kila kitu wachezaji, lakini kama wangekuwa hawana morali ya kupigania timu kutoka moyoni ingekuwa kazi bure kwa hilo Pablo amefanya kazi kubwa,” alisema Barbara na kuongeza;

“Amerudisha hali ya ushindani kwa kila mchezaji na kuna nyakati amekuwa akitueleza aina ya wachezaji tunaotakiwa kuwa nao hata ikifikia wakati wa usajili tuchukue wa aina hiyo.”

Pablo amesema hata timu zilizokuwa zikiichukulia poa Simba kwa sasa zinafikiria mara mbilimbili zinapojua zinakutana na Simba na kwamba anaamini moto huo utaendelea kwenye michezo yao yote iliyosalia ya Ligi Kuu Bara ikiwamo dhidi ya watani wao itakayopigwa Aprili 30 na zile za michuano ya ASFC iliyopo hatua ya Robo Fainali sambamba na michezo ya yao ya CAF.

SOMA NA HII  SIMBA SC IMEPANIA KURUDISHA UFALME WAKE BAADA YA KUKOSA MATAJI.... LEO KLABU YA SIMBA IMEMTANGAZA MCHEZAJI WAKE HUYU MPYA

“Katika vipindi tofauti Pablo amekuwa akiwafuatilia wachezaji na kuishi nao kama familia yake wanapokuwa kambini hata nje ya kambi ili kuona kila mmoja anaishi katika mazingira gani. Nimekuwa nikifanya naye vikao vya mara kwa mara na amekuwa akinipatia ripoti ya kile alichotaka kufanya kwenye muda uliopita, alipofaulu pamoja na walipokuwa na changamoto na vipi atakwenda kuboresha pamoja na programu ambayo atafanya kwa muda unaofuata,” alisema Barbara.

“Kuna maboresho na mambo ya kiufundi ambayo amekuwa akihitaji kutoka kwetu na kama viongozi tumemuahidi kumpatia vyote kwa wakati ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika kila mashindano.”

Katika hatua nyingine Barbara alisema kama viongozi wao wamewekeza nguvu zaidi katika mechi zao na kuona namna gani watafanya vizuri bila ya kuangalia mpinzani wao amefanya nini kwa wakati huo.

“Bado tupo katikati ya vita, tunaendelea kupambana na washindani wetu ila mwisho wa msimu kwenye mashindano yote itafahamika Simba tumefanikiwa katika maeneo gani,” alisema Barbara aliyesimamia mchakato wa kumleta Pablo nchini.

Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiachwa pointi 11 na vinara Young Africans.