Home Habari za michezo CHAMA ‘APIGA CHINI’ MAAGIZO YA PABLO SIMBA…MHILU KAKOLANYA NA BWALYA WAONYESHA MFANO…

CHAMA ‘APIGA CHINI’ MAAGIZO YA PABLO SIMBA…MHILU KAKOLANYA NA BWALYA WAONYESHA MFANO…


Mshambuliaji Yusuph Mhilu alikuwa mchezaji wa kwanza kutinga kambi ya Simba iliyoanza baada ya mapumziko mafupi ya siku tano, huku kiungo Clatous Chama akikwama kutua kwa wakati tofauti na alivyotaka kocha Pablo Franco.

Kocha Pablo aliwataka wachezaji wote kurudi kambini kabla ya chakula cha mchana wa juzi na Mhilu alikuwa wa kwanza akifuatiwa Ally Salim, Beno Kakolanya na Rally Bwalya, lakini ikaelezwa Chama alishindwa kutua nchini jana kutoka Zambia na badala yake aliingia jana kuungana na wenzake.

Mastaa wa Simba waliwasili kambini kwao Mbweni kabla ya chakula cha mchana na jioni walikwenda mazoezini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN, ambayo Chama hashiriki hata hivyo.

Awali, baada ya kuwasili nchini wakitokea Benin, Pablo aliwapa mapumziko ya siku tano wachezaji wake na kuwaambia anawataka wote kambini Machi 27, wapate chakula cha mchana kisha kwenda mazoezini na juzi ndio ilikuwa hivyo.

Mchezaji wa kwanza kufika kambini kama Pablo alivyokuwa akihitaji alikuwa winga, Yusuph Mhilu aliyewasili saa 5 asubuhi na baada ya hapo wakafuata, Ally Salum, Kakolanya na Bwalya waliokuwa kwenye nne bora na wengine kufuata.

Baada ya wachezaji wengine wa Simba kufuata nyuma saa 7:15 mchana walipata chakula cha mchana, kisha kila mmoja alikwenda chumbani kwake kwa ajili ya kuweka mambo yake sawa ili kwenda mazoezini jioni yalioanza saa 10:30 kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena.

Kwa kuwa walikuwa na mapumziko ya siku tano kabla ya kwenda mazoezini, Pablo aliwaita wachezaji na wasaidizi wake kufanya kikao kifupi kwa ajili ya kuwaeleza umuhimu wa mazoezi na mchezo ulio mbele yao.

Wakati hayo yote yakiendelea, kiungo fundi Mzambia Chama hakuwa sehemu ya kikosi kilichoingia kambini juzi kwani ndio alikuwa anaanza safari ya kutoka kwao kwa ajili ya mambo ya kifamilia. Chama hatumiki na Simba kwenye michuano ya CAF sababu awali aliitumikia RS Berkane ya Morocco aliyojiunga nayo mwishoni mwa msimu uliopita kabla ya kurejea Msimbazi kwenye dirisha dogo la usajili.

SOMA NA HII  SIMBA SC "MECHI NA HOROYA NI USHINDI TU"...HUU HAPA UNDANI WA MAANDALIZI ...KIBU YUPO FIT

Kabla ya kikosi cha Simba kwenda Benin Chama aliomba ruhusa ya kwenda Zambia kwa ajili ya kuweka sawa mambo yake ya kifamilia na alitarajiwa kuwasili nchini jana kwani alianza safari ya kurejea juzi.

Aidha, nyota waliokuwa katika kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars nao waliungana na wenzao juzi, baada ya kocha Kim Poulsen kumkubalia Pablo alipowaomba.