Home Habari za michezo UKWELI NI KWAMBA….USHINDI WA SIMBA JUMAPILI UTAIBEBA TENA TANZANIA CAF…ISHU NZIMA IKO...

UKWELI NI KWAMBA….USHINDI WA SIMBA JUMAPILI UTAIBEBA TENA TANZANIA CAF…ISHU NZIMA IKO HIVI…


Zimebaki siku tano tu kabla ya Simba kujua hatma yake katika ushiriki wa michuano ya kimataifa kwa msimu huu wakati itakapovaana na US Gendarmarie (USGN) ya Niger katika mechi ya mwisho ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo itakayopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kutinga robo fainali kuungana na wababe wengine saba, lakini utamu ni kwamba kama itapenya hapo, basi itaendelea kuzibeba klabu nyingine kushiriki michuano ya CAF kwa msimu ujao.

Ndio, kama Simba itatinga robo fainali itaendelea kuipa neema Tanzania Bara kuwakilishwa na timu nne kama ilivyokuwa msimu huu, kwa maana mbili zitakipiga Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine kama hizo zitacheza Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa mfumo wa kuhesabu pointi unaotumika kutoa uamuzi wa idadi ya timu ambazo zitawakilisha nchi katika mashindano ya klabu yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Tanzania Bara itakuwa na nafasi kubwa ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya klabu Afrika msimu ujao ikiwa Simba itatinga robo fainali.

Hadi sasa Tanzania ina alama 23 ambazo zitaongezeka hadi kufikia 30.5 iwapo Simba itafika robo fainali na itapanda kutoka nafasi ya 12 iliyopo hadi ya nane, tisa au kumi kati ya nchi 12 zinazopewa fursa ya kuingiza timu nne kila moja kulingana na mafanikio ya klabu za nchi za Zambia, Libya na Nigeria.

Nigeria kwa sasa ina alama 26 na haina timu hata moja kwenye hatua ya makundi ya michuano ya CAF, hivyo italazimika kuipisha Tanzania huku Zambia yenye pointi 24.5 imekalia kuti kavu kwa vile Zanaco inashika mkia katika kundi A ikiwa na pointi tatu.

Tanzania inapaswa kuiombea mabaya Zanaco imalize mkiani mwa kundi lake ili Zambia ibakie na pointi 24.5 ilizonazo sasa tofauti na iwapo itamaliza ikiwa nafasi ya tatu ingawa timu hiyo ya Zambia hata ikipata ushindi katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Pyramids FC haitaweza kufuzu robo fainali.

SOMA NA HII  AHMED ALLY:- MAMBO MAKUBWA HUFANYIKA USIKU...HAKUNA WAKUTUZUIA...

Libya ni tishio zaidi kwa Tanzania katika kinyang’anyiro hicho kwani hadi sasa ipo nafasi 13 na ina pointi 23 sawa na Tanzania huku ikiwa na wawakilishi wawili katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao ni timu za Al Ahli Tripoli na Al Ittihad Tripoli.

Al Ahli Tripoli kwa sasa inaongoza kundi A ikiwa na pointi 10 na tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali wakati Al Ittihad yenyewe ina nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali kwani inashika nafasi ya pili katika kundi B ikiwa na pointi 10 wakati JS Saoura inayoshika nafasi ya tatu ina pointi saba.

Tanzania pia inapaswa kuomba timu ya Cotonsport inayoshika mkia katika kundi C imalize nafasi hiyo hadi hatua ya makundi itakapomalizika ili nchi hiyo yenye pointi sita hadi sasa isipate nafasi ya kuinyemelea.

Kama Asec Mimosas ya Ivory Coast itaongoza kundi D na kufuzu robo fainali inaweza kuwa tishio kwa Tanzania iwapo itatinga hatua ya fainali au kutwaa ubingwa itaikaribia Tanzania.

Simba inashika nafasi ya tatu kwenye kundi D na inatakiwa kupata ushindi kwenye mechi ya mwisho Aprili 3 dhidi ya US Gendarmerie ambao utaifanya ifikishe jumla ya pointi 10 na kutinga robo fainali.

Hadi sasa timu tano zimeshatinga robo fainali ambazo ni Al Ahli Tripoli na Pyramids za kundi A, Orlando Pirates ya kundi B na nyingine mbili ni za kundi C ambazo ni Al Masry na TP Mazembe.

MSIKIE BOCCO

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema kuwa watahakikisha wanatinga robo fainali kwa ajili ya heshima ya nchi: “Tunajipanga kwa mechi yetu ya mwisho ya nyumbani ninaamini tutawapa furaha mashabiki wetu kwa kutimiza lengo la kuingia robo fainali.”