Home news CHAMA LA SAMATTA LAWANIA UBINGWA UBELIGIJI…KELVIN JOHN MAMBO BADO..GENK TAABANI..

CHAMA LA SAMATTA LAWANIA UBINGWA UBELIGIJI…KELVIN JOHN MAMBO BADO..GENK TAABANI..


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anakaribia kucheza mchujo wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ akiwa na chama lake Royal Antwerp F.C.

Kabla ya mchezo wa juzi ambao walikuwa wakicheza ugenini dhidi ya Anderlecht, walikuwa nafasi ya tatu wakiwa na pointi 56 walizokusanya kwenye michezo 30 kwa kushinda 17, sare mitano huku wakipoteza mara nane tu msimu huu.

Ikiwa imesalia michezo minne kabla ya duru la pili la Jupiler Pro kumalizika, Royal Antwerp F.C. anayoichezea Samatta sambamba na Union Saint-Gilloiseni, Club Brugge ndizo timu nne zilizo kwenye nafasi ya kucheza mchujo wa kuwania ubingwa huo.

Jupiler Pro ni tofauti kidogo na ligi nyingine nyingi kwani muundo wa uchezaji wao mara baada ya kila timu kucheza michezo yake yote ya msimu, huingia kwenye hatua ya lala salama hapo kuna mgawanyo wa makundi matatu.

Kundi la kwanza litajumuisha timu ambazo zimemaliza kwenye nne bora hizo zitacheza ligi yao na atakayevuna pointi nyingi ndiye atakayetawazwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, kundi jingine litakuwa na kibarua cha kuwania tiketi ya kucheza Europa Ligi msimu ujao, na la mwisho ni kujinasua kushuka.

Kimahesabu Royal Antwerp wanahitaji ushindi kwenye michezo yao mitatu kati ya minne iliyosalia ili kutinga kwenye mchujo wa ubingwa. Mechi hizo zilizosalia ni dhidi ya Anderlecht (juzi), Zulte Waregem (nyumbani), OH Leuven (ugenini) na Cercle Brugge (nyumbani).

Kama chama la Samatta litafikisha pointi 65 kwa kushinda michezo hiyo, inamaana hakuna timu kati ya zinazoshika nafasi ya tano kushuka chini ambayo inaweza kuwaondoa kwenye zile ambazo zitamaliza nne bora.

Wakati mambo yakimnyookea Samatta akiwa na chama lake hilo ambalo analichezea kwa mkopo wenye kipengele cha kusajiliwa moja kwa moja, timu ya zamani ya mshambuliaji huyo nchini humo, Ubelgiji, KRC Genk yenyewe mambo sio shwari kwani wapo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Wao huenda wakapata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu nne ambazo zitamaliza kuanzia nafasi ya tano hadi ya nane kwa ajili ya kupigania nafasi ya kucheza Europa Ligi msimu ujao hata hivyo wanapaswa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michezo yao iliyosalia ili wasishushwe nafasi hiyo.

SOMA NA HII  AZAM WAJIFUA TUNISIA KWAAJILI YA YANGA

Ikumbukwe kuwa Samatta anaichezea Royal Antwerp kwa mkopo akitokea Fenerbahce, mkopo wenye kipengele cha kusajiliwa moja kwa moja na klabu hiyo endapo akiwavutia kabla ya mchezo wa juzi, nahodha huyo wa Taifa Stars, akaunti yake ya mabao ilikuwa inasoma manne huku akitoa asisti nne kwenye ligi.

Kiujumla Samatta amefunga mabao manane kwenye mashindano yote tangu arejee Ubelgiji ambako msimu wa 2018/19 alitwaa ubingwa wa Jupiler Pro.

ISHU YA KELVIN ILIVYO

Licha ya kupandishwa rasmi kwenye kikosi cha kwanza cha KRC Genk huko Ubelgiji, inaelezwa kwamba, Kelvin John ‘Mbappe’ ataendelea kutumika kwenye michezo mbalimbali ya timu za vijana chini ya miaka 21 na 18 kwa ajili ya kuendelea kuwa fiti kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa sasa Genk wapo kwenye presha ya kuhakikisha wanamaliza vizuri msimu hivyo ni ngumu kwa kinda huyo wa Kitanzania kuanza kupata nafasi ya kucheza moja kwa moja kwenye kikosi hicho cha kwanza ambacho amekuwa akifanya nacho mazoezi.