Home news CHICO USHINDI, BACCA NA KIBWANA WAMTIA ‘WAZIMU’ WA GHAFLA NABI..VIWANGO VYAO MHHH…

CHICO USHINDI, BACCA NA KIBWANA WAMTIA ‘WAZIMU’ WA GHAFLA NABI..VIWANGO VYAO MHHH…

 


YANGA juzi imecheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Somalia na kutoka nao sare ya bao 1-1, huku baadhi ya nyota waliokuwa nje ya uwanja kwa matatizo mbalimbali ikiwamo majeraha, kama Kibwana Shomary, Chico Ushindi na Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ wakirejea na kumpa mzuka Kocha Nasreddine Nabi, aliyesema sasa jeshi lake linaenda kambini kujiandaa na ‘fainali’ dhidi ya KMC.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, Chico Ushindi alifunga bao lake la kwanza akiwa na uzi wa Yanga kwa kumalizia kwa kichwa krosi tamu ya beki Djuma Shaban, huku kocha Nabi aliwatumia wachezaji wengi waliokuwa nje katika dakika 45 za kwanza.

Nabi alisema mchezo dhidi ya Somalia umewapa kipimo kizuri kuwaangalia wachezaji ambao walikuwa wanarejea kutoka katika maumivu lakini sasa wanarudi kazini kuanza kuangalia mechi zao za mashindano.

“Tumewaona wachezaji ambao wanarejea tumewapa nafasi na kila kitu kimeonekana matokeo sio kitu cha muhimu, japo hatujapoteza lakini siwezi kusema kama nimeridhishwa na kiwango chao,” alisema Nabi aliyewatumia Bacca, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, straika Heritier Makambo na Chico Ushindi.

Nabi alisema kurudi kwa wachezaji hao kumempa faraja kubwa na kwamba wanaenda sasa kambini kujiandaa mithili ya kwenda kucheza mchezo wa fainali dhidi ya KMC ambao msimu uliopita kuna hesabu waliiharibia Yanga.

Kocha huyo ambaye hajaonya machungu ya kipigo msimu huu alisema mchezo wao dhidi ya KMC utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kupoteza mchezo uliopita walipokubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union.

“Tunapokutana na KMC siku zote imekuwa mechi ngumu kwetu, tunakwenda kujiandaa kucheza fainali nafikiri mliona wapinzani wetu walipoteza mechi iliyopita hawatataka kukubali kupoteza mara mbili mfululizo,” alisema Nabi na kuongeza;

“Mchezo kama huu msimu uliopita unathibitisha kwamba timu hizi zinapokutana hali ya ushindani inakuwaje,kwahiyo tunatakiwa kujiandaa sawasawa ili tuzidi kubaki salama katika malengo yetu.”

Katika mchezo wa kwanza msimu huu Yanga iliipiga KMC kwa mabao 2-0, lakini msimu uliopita timu hizo zilimalizana kwa sare ya bao 1-1 matokeo ambayo yalizidi kuwaondoa Yanga katika mbio za ubingwa.

SOMA NA HII  KOCHA WA SIMBA SC KUKUTANA NA YANGA NUSU FAINAL CAF...WASAUZI MENO NNJEE...

Timu hizo zitakutana Machi 19 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa 18 katika ligi kwa timu zote ambapo Yanga itataka kuendeleza kasi yake kwenye ligi huku KMC ikitaka kubadili upepo baada ya mshtuko waliupata kutoka kwa Coastal Union.

Yanga yenye pointi 45 kileleni haijafungwa katika Ligi Kuu Bara tangu Aprili 25 mwaka jana ilipolazwa na Azam kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Prince Dube na imefikisha jumla ya mechi 24, zikiwamo saba za msimu uliopita na 17 za msimu huu bila kuonja machungu ya kufungwa.