Home news BAADA YA KUWAKOSA WAARABU…BOCCO ASHUSHA ‘PRESHA’ SIMBA..DAKTARI AFUNGUKA A-Z…

BAADA YA KUWAKOSA WAARABU…BOCCO ASHUSHA ‘PRESHA’ SIMBA..DAKTARI AFUNGUKA A-Z…


NAHODHA wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ ameshusha presha ya mashabiki wa timu hiyo baada ya kuwatoa wasiwasi kuhusu afya yake baada ya kuumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.

Bocco hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichocheza dhidi ya RS Berkane katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani tangu alipoumia kwenye mchezo ambao Simba ilishinda mabao 2-0 alipewa mapumziko ili kusikilia hali yake.

Hata hivyo, juzi Bocco alisema hali yake ipo vyema na jeraha alililolipata halikuwa tishio baada ya kufanyiwa vipimo na madaktari kabla ya kupewa mapumziko na kwamba ataungana na wenzake baada ya mechi hiyo ya jana iliyopigwa jijini Dar.

Alisema anashukuru Mungu maendeleo yake ni mazuri tofauti na alivyokuwa siku ya kwanza alivyopata hiyo shida na kushindwa kuendelea na mechi ile ya Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere aliyefunga bao la pili kwa kichwa.

“Nilishtua nyama za paja ila kiukweli maendeleo yangu ni mazuri kabisa nitaungana na wenzangu siku si nyingi,” alisema Bocco aliyecheza Ligi Kuu kwa misimu 14 tangu 2008 akifunga jumla ya mabao 139, japo msimu huu hadi sasa hajafunga bao la ligi.

Naye Daktari wa Simba, Edwin Kagabo alikiri ni kweli Bocco hakucheza jana kutokana na maumivu aliyoyapata katika mechi ya Dodoma, lakini hali yake ipo freshi kwani walimpatia matibabu ya haraka mara alipotolewa uwanjani.

“Tulimpatia siku za kupumzika ili kuangalia maendeleo yake na kile ambacho kinamsumbua ila baada ya kumuangalia vizuri zaidi kitaalamu hakuwa amepata shida kubwa,” alisema Kagabo na kuongeza;

“Alishtua nyama za nyuma ya paja na kwa mapumziko aliyopata na matibabu aliyofanya matumaini yetu tutakuwa naye mazoezini baada ya mechi ya Berkane ila hana shida kubwa ya kumfanya kuwa nje zaidi.”

SOMA NA HII  SAMATTA AFUNGUKA 'ALIVYOJIKAZA KISABUNI' NA PESA ZA TP MAZEMBE...ADAI ANGEKUWA CHIZI...