Home Habari za michezo LUSAJO: – MSINISHINDANISHE NA MAYELE…MNANIPA PRESHA…,UNAWEZA UKAPATA MAJERAHA…

LUSAJO: – MSINISHINDANISHE NA MAYELE…MNANIPA PRESHA…,UNAWEZA UKAPATA MAJERAHA…


STRAIKA wa Namungo na Timu ya Taifa, Taifa Stars, Reliants Lusajo amesema kushindanishwa na Fiston Mayele wa Yanga kumesababisha awe na presha kubwa, huku baadhi ya mashabiki wakitarajia makubwa kutoka kwake wakati lengo lake ni kuisaidia timu yake na si kushindana na mtu.

Lusajo ambaye ana mabao 10 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, sawa na Mayele, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amesema kuwa kutokana na Mayele kuwa anafunga, basi baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimshinikiza afunge au kufanya makubwa zaidi, kitu ambacho hakikuwahi kumtokea huko nyuma.

“Unajua mimi sishindani na mtu kwa sababu lengo si kushindana, mimi nafunga mabao kwa ajili ya kuisaidia timu yangu na misimu yote hii nimekuwa nafunga, lakini msimu huu watu wamenifanya niwe na presha ili kushindana na Mayele, mimi kufunga ni kawaida yangu na wala silali na kuwaza kuwa nakwenda kufunga au najiandaa sana, hapana, unajua vitu vingine ni asili tu, kwa hiyo sina wasiwasi nitafunga sana, ila si kushindana na mtu,” alisema Lusajo.

Kuhusu Mayele anasema kuwa anamheshimu sana straika huyo, kwa sababu naye pia ametokea kumheshimu, hivyo wote wawili wanaheshimiana.

“Mayele ni straika mzuri sana na tunaheshimiana sana, lakini mimi pia nawaheshimu mastraika wengine kama George Mpole, John Bocco na Meddie Kagere. Unajua Bocco na Kagere lazima uwape heshima ya pekee kwa sababu wamefanya vitu vikubwa kwenye ligi yetu na nje ya nchi ambavyo sisi wenyewe bado hatujavifanya,” alisema.

Akizungumzia Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu Bara, alisema hafikirii sana hilo, lakini pia akaongeza mchezaji yeyote si lazima wao, anaweza kuwa mfungaji bora.

“Huu ni mpira bwana, unaweza kuongoza, ukapata majeraha, ukakaa nje, wakaja wengine wanafunga wakawa wafungaji bora,” alisema Lusajo ambaye amewahi pia kuichezea KMC.

Aidha, Lusajo alisema siri kubwa ya mafanikio yake katika kufunga ni kumsikiliza kocha wake kwa makini nje na ndani ya uwanja.

“Kinachonifanya nifanye vizuri ni kule kumsikiliza kocha wangu kwa makini pamoja na kushirikiana na wachezaji wenzangu,” alisema Lusajo.

SOMA NA HII  HII HAPA MASHINE YA KAZI ILIYOIKATAA YANGA NA KUKIMBILIA PESA ZA WAARABU..ISHU IKO HIVI...