Home news MOTO WA MAYELE NDANI YA YANGA WAWATOA UDENDA WACONGO….WAOMBA KUSAJILIWA…

MOTO WA MAYELE NDANI YA YANGA WAWATOA UDENDA WACONGO….WAOMBA KUSAJILIWA…


KIWANGO cha juu alichokionyesha straika wa Yanga, Fiston Mayele, hakijampa jina kubwa na kuimbwa na mashabiki wa soka nchini tu, kumbe hadi nyumbani kwa DR Congo jamaa amewashtua na kuwafanya Wakongo wenzake kuanza kuingia mtegoni na kutaka kuja Tanzania kukiwasha.

Mayele amefunga mabao 10 na kuasisti mara tatu akiwa kinara wa mabao wa Yanga na kwenye msimamo wa orodha ya wafungaji akiwa sambamba na Reliants Lusajo wa Namungo, pia akiwa amezawadiwa ng’ombe wawili, huku jina lake likiimbwa na kuwadatisha mashabiki kwa staili yake ya kushangilia iliyo gumzo hadi makanisani.

Mafanikio ya nyota huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo, imewashtua Wakongo na kocha wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu amesema kuwa wachezaji wengi wakubwa katika ligi ya kwao wamekuwa wakishangazwa na jinsi jina la Mayele na wenzake linavyopaa na kuwa na mashabiki wengi.

Shungu alisema wachezaji hao wamekuwa wakiulizia jinsi malipo ya klabu za Tanzania wakitaka kuja kucheza soka nchini wakivutiwa na jinsi wenzao wakiongozwa na Mayele wanavyowika.

“Hapa sasa wachezaji wengi wanaulizia sana juu ya maisha ya Tanzania wamevutiwa sana na Mayele jina lake lilivyokua kubwa huku wakiona katika mitandao wanashangaa sana,” alisema Shungu aliyeifundisha Yanga kwa mafanikio kati ya 1998-2001 ikiwamo kuwapa ubingwa wa Kombe la Kagame 1999, michuano iliyofanyika Uganda.

Kocha huyo pia aliyeiongoza Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi mwaka 1998 akimpokea aliyekuwa Kaimu Kocha Mkuu, Tito Mwaluvanda, alisema Yanga na Simba kama zikiweka mtandao mzuri zitakuwa na nafasi kubwa ya kupata mastaa wazuri kutoka Congo kutokana na kuona mafanikio ya wenzao huku pia wakivutiwa na mashabiki wanavyopenda wachezaji wao.

Alisema ligi ya DR Congo ilipepesuka kidogo ingawa bado wachezaji wanalipwa fedha ndefu kuliko malipo ya klabu za Tanzania.

“Hizi klabu kubwa za Yanga na Simba kama zikiwa na watu wazuri wa kuwatafutia wachezaji, watawachukua wengi sana, naona Yanga wamepata hao watu ndio maana unaona sasa timu yao ina wachezaji bora wa kutoka huku, hapo Tanzania shida inabaki kuwa moja kiwango cha malipo ya mishahara.

SOMA NA HII  WINGA TELEZA WA TP MAZEMBE AKUBALI KUTUA YANGA...NI YULE ALIYEMTESHA ULIMI DJUMA

“Hapa Congo bado wanalipwa fedha nyingi kushinda Tanzania lakini wachezaji wa hapa wanapenda kuzichezea klabu zenye mashabiki wengi kama zilivyo hizi Yanga na Simba.”

Mayele katika mechi 17 alizocheza hadi sasa katika ligi amehusika katika mabao 13 na kuisaidia Yanga kuwa kileleni mwa msimamo ikiongoza kwa alama 45, ikiizidi Simba ambayo ni watetezi wa taji wakiwa nafasi ya pili na alama zao 37 na kuwapa matumaini mashabiki kwamba msimu huu chama lao litabeba ubingwa.