Home Habari za Simba OSCAR OSCAR – KILA KITU KUHUSU ZIMBWE Jr KINAVUTIA…CHAMA ANAFANYAGA MAMBO YASIYO...

OSCAR OSCAR – KILA KITU KUHUSU ZIMBWE Jr KINAVUTIA…CHAMA ANAFANYAGA MAMBO YASIYO NA MSINGI..


BINAFSI ni shabiki mkubwa sana wa staa wa timu ya taifa ya Tanzania, Mohammed Hussein. Siyo yule ‘Mmachinga’ wa zamani wa Yanga bali beki wa kushoto wa sasa wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala.’

Mara zote ananifurahisha ninapomtazama ‘akipaa’ na mpira katika upande wa kushoto wa Simba.

Tshabalala ni kati ya wale wachezaji wachache ambao huwezi kuwachukia hata kama hawachezi katika timu yako. Unamchukia Tshabalala siku moja tu! Siku anapocheza dhidi ya timu yako.

Hawapo mabeki wengi nchini kama Tshabalala. Sijui tuseme mabeki wengi au wachezaji wengi? Vyovyote vile anavutia kwa mambo mengi. Nitakueleza kadhaa.

Tatizo kubwa zaidi la Watanzania ni kutaka kuharakisha mambo. Si katika soka tu bali katika maisha ya kawaida. Tunapenda kufanya mambo mengi kwa haraka. Tunataka daladala ziende mwendo kasi ili tuwahi kufika.

Tunataka tuhudumiwe haraka dukani, hospitalini na maeneo mengine yanayohitaji utaratibu. Hatutaki kupanga foleni kuingia viwanjani.

Tunaamini foleni inatuchelewesha. Kwa kifupi hatuamini kwenda taratibu ni sehemu ya maisha. Hilo limeathiri hadi wachezaji wetu.

Muda mwingine sehemu ya kutulia na kupiga pasi rahisi, mshambuliaji wa Tanzania atalazimika kupiga shuti kubwa golini kisa majukwaa yanataka apige, pia yeye mwenyewe anahitaji kuwahi kuipatia timu yake bao. Muda mwingine beki atalazimika kubutua mpira mbele kwa kuhofia kupokonywa na mshambuliaji. Watanzania hawaamini mpira unafika mbele haraka mkianzia mpira nyuma. Ni kwa sababu hatujazoea maisha ya utulivu.

Watanzania wote tukiwa tunazidi kwenda haraka na maisha, Tshabalala hayupo hivi uwanjani. Mara zote hafanyi ambacho majukwaa wanahisi ni sahihi, yeye hupenda kufanya anachoamini ni sahihi.

Katika eneo ambalo mashabiki wanaweza kudhani maamuzi sahihi ni kupiga krosi, yeye anaweza kuamua kupiga chenga au kpiga pasi salama.

Mchezaji hupaswi kuendeshwa na majukwaa. Unapaswa kufanya unachokiamini ni bora kama anavofanya Tshabalala.

Mchezaji mwingine mwenye utulivu kama Tshabalala ni Clatous Chama wa Simba. Huwa hafanyi ambacho mashabiki wanaamini ni sahihi hasa wanaposhambulia. Kuna muda anafanya mambo yasiyo na msingi kama kupiga kanzu na tobo lakini wanaposaka bao hufanya mambo anayoamini ni sahihi.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA PILI SAUZI...DYLAN KERR AIPA SIMBA MBINU ZA KUIMALIZA ORLANDO MAPEMA...

Tabu kubwa ya mastaa wengi wa Tanzania ni nidhamu. Wachezaji wengi wanapofika Simba na Yanga na kuibuka kuwa vipenzi vya mashabiki wanachomoa kucha zao na kuanza kusumbuana na vilabu vyao.

Wanafahamu watapata utetezi wa mashabiki na viongozi. Wanatokea wachache wanaoweza kuishi kama mastaa na kuendelea kuwa na nidhamu. Katika miaka takribani nane niliyomfahamu Tshabalala ndani ya Simba sijasikia akifanya matukio ya utovu wa nidhamu. Sijawahi kusikia ametoroka kambini au ameacha kuhudhuria mazoezi. Ni mchezaji mstaarabu nje ya uwanja kama alivyo ndani ya uwanja.

Nakumbuka msimu fulani aliosota benchi pale Simba baada ya kuibuka beki wa kushoto wa Ghana, Kwasi Asante. Msimu mmoja nyuma Tshabalala alikuwa beki bora wa kushoto nchini lakini alipata majeraha katika fainali ya kombe la FA kule Dodoma, ilimchukua muda kurejea.

Kwasi aliitumikia nafasi yake vyema na Tshabalala alisahaulika. Baada ya msimu mmoja Tshabalala alirejea kuchukua nafasi yake na kumweka Kwasi Asante benchi.

Mwaka mmoja mbele Simba hawakuwa na la Zaidi la kufanya Zaidi ya kuachana na Kwasi. Hapo tunajifunza kumbe wapo wachezaji wazawa wanaoweza kuwapoteza wachezaji wageni.

Kumbe kinachoikwamisha timu ya taifa si idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni wanaokuja kucheza ligi kuu bali ni kwasababu hatuna wachezaji wengi wazuri.

Tungekuwa na wachezaji wazuri wageni wasingeletwa nchini. Mbona Simba hawafikirii kumleta mgeni kwenye eneo la Tshabalala?

Kati ya vingi vinavovutia kwa Tshabalala ni jinsi alivyofanikiwa kutengeneza kipato kupitia jina lake. Katika mtandao wa kijamii wa Instagram ana wafuasi milioni moja.

Ni mchezaji pekee ligi kuu bara mwenye idadi hiyo ya wafuasi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram anafanya matangazo yanayomuingizia kipato tofauti na mshahara anaolipwa kila mwezi na Simba.

Kupitia jina lake ana channel yake Youtube inayofanya vema. Bado anatumia jina lake kuuza fulana maarufu za M-15. Ilikuwaje Tshabalala akaweza yote haya?

Makala haya yameandikwa na Oscar Oscar na kuchapishwa awali kwenye wavuti la Mwanaspoti.