Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi yupo njiani akirejea nchini kuja kuendelea na kazi, lakini akatoa kauli tamu kwa mashabiki kwamba msimu ujao kama watachukua ubingwa anataka kutulia kutafuta mtu mwingine wa makali wa kutupia kushinda straika wake, Fiston Mayele.
Mayele ana mabao 10 kwa sasa katika Ligi Kuu Bara akilingana na Reliants Lusajo wa Namungo, akiwa pia ameasisti mara tatu, huku akiwa gumzo na tishio kubwa kwa mabeki na makipa wa timu pinzani, lakini Nabi amesema anataka mashine nyingine kali zaidi ili mambo yawe sawa.
Kocha Nabi aliyekuwa kwake Ubelgiji inapoishi familia yake, amesema anatambua ubora wa Mayele lakini anataka kuona ushindani zaidi katika eneo hilo wakati washambuliaji wengine wakiendelea kutafuta ubora wao.
Nabi aliyechukua tuzo mbili za Kocha Bora wa mwezi msimu huu aliongeza ingawa sio kazi rahisi sokoni kupata mtu bora tena kama Mayele lakini ameshaanza kufuatilia ligi mbalimbali za Afrika kusaka mtu mzuri zaidi anayejua kufunga.
Alisema lengo lake ni kuona anakuwa na chaguo pana la washambuliaji ambapo zipo mechi ambazo kuna wakati anatamani kuanza na washambuliaji wawili.
“Tuna Mayele anafanya vizuri sana lakini kama ukichukua ubingwa unajipeleka katika eneo jingine ambalo unahitaji kuwa na ubora zaidi ya huu tulionao sasa,” alisema Nabi.
“Tutahitaji mtu mwingine bora kama Mayele au zaidi, mimi naamini katika ushindani wa nafasi kwa wachezaji. Kwa sasa Mayele amebahatika kuwa na anguko la wenzake wapo ambao waliumia na wengine kutoanza vizuri.”
Yanga ilikabiliwa na majeruhi wawili katika eneo la ushambuliaji ambao ni Yacouba Songne ambaye wiki iliyopita alirejea nchini tayari kwa kuanza mazoezi mepesi.
Yacouba, hata hivyo, bado atahitaji muda zaidi kuweza kuwa sawa huku mwingine Crispn Ngushi na Yusuf Athuman wakianza kutafuta ubora wakifanya mazoezi sambamba na wenzao.
Mkongomani Heritier Makambo naye tangu msimu uanze ameshindwa kuwa chaguo la kwanza mbele ya Mayele akiwa hana bao mpaka sasa kwenye Ligi Kuu licha ya kufunga hat trick kwenye ASFC.
“Nimeanza kutafuta mtu mzuri zaidi ingawa natambua sio kazi rahisi, sio kila wakati unaweza kubahatika kupata mshambuliaji kama Mayele, washambuliaji ni wachezaji ambao wako wachache sana wenye ubora,” alisema Nabi na kuongeza;
“Kuna wakati katika mechi unatamani kuanza na washambuliaji wawili hili lazima tuanze kulifanyia kazi sasa ingawa kitu muhimu kutangulia sasa ni kuchukua ubingwa kwanza ili tubaki katika malengo yetu.”
Aidha, Nabi alichekelea kuzidi kupungua kwa idadi ya majeruhi katika kikosi chake akisema hatua hiyo itazidi kuwaimarisha katika mechi zao ngumu zinazofuata ikiwamo ya Azam itakayopigwa Aprili 6 na ile ya Simba ya Aprili 30, zinazoelezwa ndizo zenye mwanga kwa Yanga juu ya ubingwa wa ligi msimu huu.