ILI kuhakisha wanayazoea mazingira ya kucheza usiku mwingi, Kocha Mkuu wa Simba SC, Pablo Franco, juzi Ijumaa aliamua kuwapigisha mazoezi ya usiku sana wachezaji wake ndani ya Uwanja wa Mkapa wakijiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmerie.
Hiyo ni kuelekea mchezo wa leo Jumapili dhidi ya US Gendarmerie utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni wa mwisho Kundi D katika michuano hiyo ambapo Simba wanatakiwa kupata ushindi ili kutinga robo fainali.
Kabla ya jana Jumamosi Simba haijafanya mazoezi ya mwisho uwanjani hapo yaliyoanza saa 1:00 usiku, walianza juzi Ijumaa ambapo walifanya kuanzia saa 4 usiku hadi saa 6 usiku muda ambao siku hubadilika.
Katika mazoezi hayo, Simba ilikuwa na mastaa wote akiwemo Pape Ousmane Sakho, Chris Mugalu, Thadeo Lwanga na Sadio Kanoute, jambo ambalo limeamsha shangwe kwa timu hiyo kutokana na nyota hao kufanya mazoezi ya nguvu na kuonekana kuwa fiti.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema sababu kubwa ya Pablo kuomba kufanya mazoezi saa nne usiku ni kuwazoesha wachezaji mazingira ili kuendana na muda husika wa mchezo wenyewe.
“Kocha Pablo aliomba katika siku mbili kabla ya mchezo husika wachezaji kufanya mazoezi katika muda sawa na mchezo husika jambo ambalo limefanyika kwa ufasaha mkubwa, hivi sasa kikosi kipo tayari kwa mapambano.
“Nia na mahitaji yetu ni kupata ushindi ili kutinga hatua inayofuata ya michuano hii, hivyo lazima tujue nini tunafanya kwa wakati sahihi na tusiwe nje ya mifumo itakayotupa matokeo,” alisema kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), michezo yote ya mwisho ya Kundi D la michuano hiyo, itacheza muda sawa ili kuepuka mazingira ya kupanga matokeo.
Wakati Simba wakicheza na US Gendarmerie saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kule Morocco kwao itakuwa saa 2 usiku ambapo kutakuwa na mchezo kati ya RS Berkane dhidi ya ASEC Mimosas.
Katika Kundi D, ASEC inaongoza ikiwa na pointi tisa, inafuatiwa na RS Berkane yenye saba kama ilivyo kwa Simba iliyo nafasi ya tatu, huku US Gendarmerie ni ya mwisho ikikusanya pointi tano.