Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZANA NA USGN…MASTAA SIMBA WATENGEWA MAMILIONI YA PESA KUISHUSHA YANGA…

BAADA YA KUMALIZANA NA USGN…MASTAA SIMBA WATENGEWA MAMILIONI YA PESA KUISHUSHA YANGA…


Kikosi cha Simba juzi usiku kilikuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ikikata tiketi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuichapa USGN ya Niger, huku mastaa wa timu hiyo wakitamba maajabu ndio zao.

Mastaa hao walisema baada ya kudokezwa kuwa wanahesabu siku kabla ya kuanza kuzioga noti kutoka michuano ya CAF, ila kama watatoboa ndani ya siku saba ngumu watakapoipigania timu hiyo katika mechi tatu mfululizo zinazowakabili.

Pape Ousmane Sakho, Bernard Morrison ‘BM3’, Meddie Kagere na wengine wana siku saba za kibabe ili kujihakikisha wanakomba mamilioni ya fedha za bonasi kama watapata ushindi kwenye mechi hizo tatu zinazoikabili timu hiyo kuanzia Alhamisi.

Ipo hivi. Baada ya  kumaliza mechi za makundi ya michuano ya kimataifa, Simba ikitinga robo fainali ya tatu mfululizo ndani ya misimu minne ya michuano ya CAF, baada ya awali kutinga mara mbili katika Ligi ya Mabingwa 2018-2019 na 2020-2021 na kujihakikisha kukomba mamilioni ya fedha.

Kwa kufuzu hatua hiyo, Simba imejihakikisha kukomba zaidi ya Sh 813 milioni kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo.

Lakini wakati ikipigia hesabu fedha hizo, mechi tatu zilizopo mbele yao zikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho itawaongezea mkwanja mwingine ndani ya wiki moja tu, kama Sakho na wenzake wataamua kukomaa zaidi uwanjani.

Inaeleweka mabosi wa Simba huwa wanatoka bonasi ya Sh 20 milioni kwa kila mchezo ambao timu hiyo inashinda, hivyo kina Sakho na wenzake kama watapambana na kutoboa katika wiki moja tu watajihakikishia si chini ya Sh60 milioni.

Simba inatakiwa kucheza mechi mbili za Ligi Kuu ikiwamo ya kiporo dhidi ya Polisi Tanzania na zote zikipigwa ugenini kabla ya kurudi Kwa Mkapa kuumana na Pamba ya Mwanza katika mechi ya robo fainali ya Kombe la ASFC.

Kama hujui, mechi hizo zinapigwa ndani ya siku saba tu, yaani wiki moja tu, kisha Wekundu hao kutakiwa kujipanga sasa kwa mechi ya Kariakoo Derby dhidi ya Yanga itakayopigwa mwishoni mwa mwezi huu.

Simba itasafiri mapema wiki hii kwenda jijini Tanga kuvaana na Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika mechi itakayopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, kabla ya siku tatu kusogea mjini Moshi kula kiporo dhidi ya Polisi Tanzania.

Mechi ya Polisi ilikuwa ipigwe Machi 27, lakini iliahirishwa mapema na Bodi ya Ligi (TPLB) ili kupisha mechi za kimataifa za Taifa Stars na sasa itapigwa Aprili 10 kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi.

Mechi hizo mbili ni muhimu kwa Simba kwani ndizo zinazoweza kuifanya ipunguze pengo la pointi dhidi ya watani wao, Yanga inayoongoza msimamo na itakayocheza Jumatano hii dhidi ya Azam FC, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.

SOMA NA HII  MAYELE ATOBOA SIRI ZA MAZEMBE...KOCHA YANGA ALIMTUMA MISHENI YA SIRI

Kama Simba itavuna pointi sita za mechi hizo itaifanya ifikishe jumla ya pointi 43 na kuikaba Yanga, ambayo ndani ya mwezi huu itacheza mechi mbili tu za Ligi Kuu dhidi ya vigogo wenzao, Azam na Simba.

Kwa sasa Yanga ina pointi 48 kutokana na mechi 18 na kuweka pengo la alama 11 baina yao na Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi zao 37 baada ya kucheza mechi 17.

Mara baada ya mechi hizo mbili za ugenini za Ligi Kuu Bara, Simba itarudi jijini Dar na siku ya tatu yake itashuka tena uwanjani kuvaana na Pamba katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la ASFC utakaopigwa Aprili 13.

Simba itacheza na Pamba muda mfupi kabla ya Azam kumalizana na Polisi Tanzania na wekundu hao watahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa baada ya kushikilia kombe kwa misimu miwili mfululizo.

Msimu uliopita ilibeba taji hilo kwa kuinyuka Yanga katika fainali tamu iliyopigwa Julai 25, mjini Kigoma kwa bao la kiungo Taddeo Lwanga.

Nyota wa timu hiyo mapema walisisitiza kuwa, wanajua mechi ya jana ilikuwa ngumu na hata zilizopo mbele yao ni ngumu zaidi, lakini maajabu kwao ni kawaida wakirejea matukio waliyowahi kuyafanya kimataifa na hata ligi ya ndani.

“Kama tuliweza kupindua meza kwa AS Vita, Nkana Red Devils na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo kwa kupindua meza, hatuoni cha kutuzuia kufanya tena safari hii,” alisema Shomary Kapombe siku moja kabla ya mechi hiyo ya jana.

Naye Kocha Pablo Franco mapema alikiri ratiba imekuwa ni changamoto kwa vijana wake, lakini wanajipanga kuhakikisha wanaendeleza moto wao katika michuano yote wanayoshiriki kwa sasa ikiwamo kutaka kutetea ubingwa wa Ligi na ASFC.

“Tuna malengo yetu msimu huu, kuona Simba tunatetea mataji yetu na hatutatimiza hilo kama hatutafanya vizuri kwenye mechi zetu, japo wachezaji wanachoka kwa kucheza mfululizo, ila tunashukuru majeruhi wamepungua,” alisema Pablo kabla ya pambano lao la jana dhidi ya USGN katika michuano ya CAF.

Simba na Yanga zitakutana Aprili 30, katika Kariakoo Derby ya 108 tangu zianze kukutana katika mechi za Ligi ya Bara iliyoasisiwa mwaka 1965. Katika mechi yao ya kwanza msimu huu timu hizo zilitoka 0-0.